2015-12-11 08:49:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio Mwaka C


Mpendwa mwana wa Mungu, tukiendelea kwa furaha katika Majilio, leo tunaendelea kulitazama Neno la Mungu kwa furaha ili tujifunze na kuonja upendo wa Mungu kwa njia ya Neno wake. Ni Dominika ya III ya Kipindi cha Majilio, Mwaka C wa Kanisa, tukialikwa kufurahi kwa uchangamfu kwa maana Bwana yu karibu. Kama kawaida Dominika ya III ni Dominika ya furaha, kumbe, furahini katika Bwana. Katika Dominika hii tunatafakari Neno la Mungu pia tukimtazama Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi wa Bwana.

Baba huyu anayo sifa ya pekee ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuishikilia daima, nayo ni UADILIFU. Mtakatifu Yosefu anamchukua Mama Bikira Maria akiongozwa na Roho Mtakatifu na anafanya kazi ya kuitunza Familia Takatifu kama Mungu alivyotaka. Daudi anampa Yesu Kristu mahali pake katika nasaba ya Daudi. Mtakatifu Yosefu ni yule ambaye anatufundisha kuwa wazi mbele ya maongozi ya Mungu, kutekeleza mapenzi ya Mungu bila kuweka vikwazo na hivi kuruhusu mpango wa Mungu usonge mbele. Mpendwa mwanatafakari wa Neno la Mungu, basi kuweni Yosefu mwingine katika familia yako ili kazi ya Bwana isonge mbele.

Katika somo la kwanza Nabii Sefania anawaalika Waisraeli kufurahi maana karibu Bwana atawaondoa katika utumwa wao, mateso na hivi watarudi nyumbani. Kwa namna hiyo Nabii ataka kutufundisha uwepo wa Mungu kati yao. Furaha hiyo ambayo anaitangaza Sefania ni furaha ambayo tulitangaziwa kwa njia ya ubatizo, yaani tulipoondolewa katika mkanda wa dhambi ya asili na dhambi nyingine zote. Ni furaha tunayoipata tunapotafakari Neno la Mungu kila siku katika jumuiya zetu. Ni furaha ya kuishi pamoja katika familia nje ya utumwa, maana katika utumwa hakuna familia bali ufisadi unaodhulumu familia.

Mpendwa nani anapenda kukaa katika utumwa na uonevu usioisha? Basi ndugu yangu furahini katika Kristu anayekualika kila siku kupokea toba na msamaha wa dhambi. Hata hivyo, ili kufurahi lazima kuiga mfano wa Mt. Yosefu mwadilifu na daraja la mapenzi ya Mungu. Tunapotafakari somo la Injili tunakutana na sura ya Yohane Mbatizaji ambaye anatoa mafundisho yake juu ya maisha ya pamoja yaani haki mgawanyo na maisha ya kumpendeza Mungu. Kuwasaidia walio maskini, kuacha dhuluma na shuru zinazozidi kiwango stahili au pangwa na wanaohusika. Pateni mishahara inayolingana na kazi zenu na walipaji wa mishahara walipe kadiri ya kazi yenyewe na maisha ya wakati huo. Nabii anafundisha juu ya jamii jinsi ya kuishi kwa ustarabu tukimwelekea Mungu.

Mpendwa haya je wayajua na wajaribu kuyaishi yaani ndiko kuishi Injili? Baada ya Nabii kufundisha hayo, ataendelea na mafundisho mengine juu ya Masiha ni nani? Anatufundisha unyenyekevu na uadilifu uleule ambao Mt. Yosefu atufundisha. Yohane Mbatizaji anasema waziwazi kuwa pamoja na hayo afanyayo yeye si Masiha bali ni sauti ya mtu aliaye nyikani akitayarisha watu wakaandae mapito ya Bwana. Tena akikazia jambo hilo anasema yule ajaye ni mkuu kiasi hawezi kugusa hata kamba za viatu vyake. Masiha ajaye ni mwenye nguvu ambaye atahukumu yote kwa haki.

Mpendwa mwaliko kwako ni uadilifu na unyenyekevu, kujishusha mpaka sakafuni mbele ya Mungu, ndiyo kusema hivi leo Kristu yu nasi kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi, kumbe kuabudu Ekaristi siyo uchaguzi bali ndiyo namna ya kumwelekea Mungu na kukaa naye. Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe Yn 1:1 na hivi kulisoma na kulitafakari kwa upole na ustadi wa kiroho ni njia za kumtukuza Mungu. Katika mwaka wa imani 2012-2013, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI alitualika akisema Neno la Mungu ndicho chakula cha Imani na chakula hiki huletwa kwa njia ya Kanisa Takatifu. Kila siku lazima kuitika na kujibu swali hili aliloulizwa Bwana “tufanye nini ili kutimiza mapenzi ya Mungu? Bwana anajibu akisema “mwamini yule aliyetumwa naye” Yn 6:28-29. Mpendwa kumwamini Mungu si kujua tu yaliyomo ndani ya imani bali kuyaishi na kuyaweka katika maisha ya watu. Kumwamini Kristu ndiyo mlango wa IMANI.

Mtume Paulo anapowaandikia wafilipi anaendelea katika Dominika hii ya furaha kukazia maisha ya furaha ambayo ni tunda la uadilifu. Si uadilifu tu bali maisha ya sala, kuwa watu wa kutoa shukrani kwa kila jambo tupokealo toka kwa Mungu na kwa wanadamu. Mt. Paulo anasema mkifanya hayo vema, amani ya Mungu itawahifadhi mioyo yenu daima. Haya basi yatutayarisha kwa kupokea furaha ijayo ambaye ni Masiha, Emanueli, Mungu pamoja nasi. Nikutakie heri na baraka tele za majilio na kipindi chote cha Noeli kiwe mwanga kwako kwa ajli ya uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.