2015-12-11 15:05:00

Marehemu Askofu mstaafu Shija kuzikwa hapo tarehe 17 Desemba 2015


Askofu mstaafu Mathayo Shija wa Jimbo Katoliki Kahama, Tanzania amefariki dunia hapo tarehe 9 Desemba 2015, wakati watanzania wakisherehekea kumbu kumbu ya miaka 54 tangu walipojipatia uhuru wao kutoka kwa Mwingereza na mwanzo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Askofu Shija alizaliwa huko Puge, Jimbo kuu la Tabora kunako tarehe 17 Aprili 1924. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre hapo tarehe 17 Januari 1954.

Kunako tarehe 11 Novemba 1983 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II akaunda Jimbo Jipya la Kahama, Tanzania na kumteua Mheshimiwa Padre Mathayo Shija kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Kahama na kuwekwa wakfu hapo tarehe 26 Februari 1984. Baada ya kuitumikia Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Kahama kwa ari na moyo mkuu, akang’atuka kutoka madarakani hapo tarehe 24 Aprili 2001. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake, apende kumpokea na kumjalia usingizi wa amani, Marehemu Askofu mstaafu Mathayo Shija wa Jimbo Katoliki Kahama, Tanzania.

Kwa ufupi, Marehemu Askofu mstaafu Mathayo Shija amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91 tangu alipozaliwa. Miaka 61 ya huduma kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kama Padre na miaka 31 ya utume wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Kahama, Tanzania. Marehemu Askofu mstaafu Shija anatarajiwa kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Kahama, hapo tarehe 17 Desemba 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.