2015-12-11 15:31:00

Fuatilieni changamoto za Papa Francisko nchini Kenya!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Kenya aliwataka waamini nchini Kenya kuwa kweli ni mashuhuda wa imani tendaji kwa kujikita katika ari na mwamko mpya wa umissionari, tayari kuwashirikisha wengine imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wananchi wa Kenya waendeleze majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi kwa ajili ya amani, ustawi na maendeleo ya wengi kwa kukataa kishawishi cha kuwa na misimamo mikali ya kiimani. 

Baba Mtakatifu  aliwataka Wakleri na watawa kuwa na kumbu kumbu endelevu, uaminifu na kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Aliwataka wananchi wa Kenya kupambana na ukabila na umaskini wa hali na kipato unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali watu na maliasili kwa ajili ya mafao ya wengi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko aliwataka wananchi wa Kenya kusimama kidete kupinga rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; kwa kuondokana na misimamo mikali ya kiimani na kuwataka vijana kuwa makini katika maisha yao, ili wasitumiwe na wajanja wachache kwa ajili ya mafao yao binafsi! Askofu mkuu Charles Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya katika mahojiano maalum na Shirika la Habari za Kanisa Afrika, CANAA anasema, ni wajibu wa Familia ya Mungu nchini Kenya kufanya tathmini ya kina juu ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya kuanzia tarehe 25 – 27 Novemba 2015, ili kuufanyia kazi ujumbe aliowaachia, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa nchini humo.

Askofu mkuu Balvo anasema huduma kwa maskini ni muhimu sana kwani hawa ndio walengwa wa Injili ya Kristo kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Familia ya Mungu nchini Kenya ilionesha ushirikiano wa dhati wakati wa maandalizi ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko na alipowasili nchini Kenya. Kulikuwepo na ugumu na changamoto mbali mbali za maisha, lakini kutokana na ushirikiano na utashi wa kisiasa, mambo yote yalikwenda kama yalivyopangwa. Watu wengi walijitokeza kumpokea, kumshangilia na kuadhimisha Mafumbo mbali mbali mbali ya Kanisa pamoja na Baba Mtakatifu. Mkutano wa vijana na Baba Mtakatifu Francisko umeacha chapa ya kudumu katika akili na mioyo ya vijana wengi nchini Kenya. Walifurahia jinsi ambavyo aliweza kugusa kwa ujasiri bila makunyanzi juu ya saratani ya rushwa, misimamo mikali ya kiimani na umuhimu wa vijana kuwa na msimamo katika maisha bila kuyumbishwa utadhani daladala iliyokatika usukani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.