2015-12-11 15:18:00

Badilini sera na misimamo yenu ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kufikia muafaka!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba,  inadhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kuwatumbukiza watu katika majanga, umaskini na magonjwa. Kumbe, kuna haja kwa viongozi wa kimataifa  kujenga utamaduni wa majadiliano kwa kusikilizana katika ukweli na haki. Wajumbe waheshimiane na kuthamiania, tayari kuonesha ujasiri wa kubadilisha sera na misimamo ili kufikia malengo yanayotarajiwa na wengi katika mkutano wa kimataifa juu ya udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa.

Kardinali Turkson ameyasema haya hivi karibuni wakati akichangia hoja kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi. Anakaza kusema, majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi ni muhimu sana kwa wakati huu ili kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi. Majadiliano yawe kigezo kikuu katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, wa kushikamana na kushirikiana kwa pamoja kama ndugu wamoja, ili kuondokana na kinzani, tayari kuambata amani na maridhiano.

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa watambue athari za mabadiliko ya tabianchi mintarafu misingi ya haki na amani. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira kwa kuwajibika barabara kwani watu wote wanaunda familia moja ya binadamu, wanaoishi katika nyumba moja, yaani mazingira ambayo yanapaswa kutunzwa vyema.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itafanya jitihada za makusudi ili kuhakikisha kwamba, muafaka unaowashirikisha wengi unafikiwa huko Paris, ili kutunza mazingira sanjari na kupambana na umaskini, ili kukuza na kudumisha utu wa binadamu. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waoneshe ujasiri kwa kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya mafao ya familia ya binadamu kwa kuonesha mshikamano unaojikita katika kanuni auni na usawa.

Kardinali Peter Tukrson, tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Waraka wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote amezunguka sehemu mbali mbali za dunia ili kuwahamasisha watu wenye mapenzi mema kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, ili kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Misingi ya haki, amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuendelea kusali ili kweli maamuzi yatakayofikiwa huko Paris, Ufaransa yawe ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; maamuzi ambayo yanatekelezeka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.