2015-12-10 10:52:00

Waraka Mpya wa Majadiliano ya Kidini kati ya Wakristo na Wayahudi


Kanisa linaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu Majadiliano ya kidini na katika ibara yake ya nne inagusia majadiliano ya kidini na dini ya Kiyahudi “Nostra aetate”. Katika maadhimisho haya, Kanisa limechapisha Waraka mpya unaogusia kwa kina na mapana, majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakristo. Waraka huu mpya kwa ufupi, unaongozwa na kauli mbiu “Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake.”

Hati hii inagusia kwa ufupi historia na umuhimu wa Waraka huu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Waraka unaangalia pamoja na mambo mengine hali ya majadiliano ya kitaalimungu kati ya Wayahudi na Wakristo. Ufunuo wa Mungu katika historia kama “Neno la Mungu linalofumbatwa katika Mapokeo ya Wayahudi na Wakristo". Kuna uhusiano wa pekee kati ya Agano la Kale na Agano Jipya. Hati hii mpya inakazia umuhimu wa wokovu kwa watu wote unaoletwa na Kristo Yesuna kwamba, Agano Kati ya Mungu na Waisraeli bado linaendelea tangu wakati ule. Dhamana ya Uinjilishaji ndani ya Kanisa mintarafu mahusiano ya Wayahudi, mwishoni, Waraka huu unabainisha malengo ya majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican miaka 50 iliyopita, walichapisha Waraka wa Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani na katika kipengele cha nne, Kanisa linaonesha kwa namna ya pekee chemchemi ya imani yake, nafasi ya Mababa wa imani, Agano la Kale linalopata utimilifu wake kwenye Agano Jipya na kwamba, Kristo ndiye amani yao aliyewapatanisha Wayahudi na Wakristo; umuhimu wa Maandiko Matakatifu pamoja na udugu wa watu wote unaojikita katika mapendo.

Waraka huu mpya unajaribu kufanya tafakari ya kina kuhusu mambo msingi yaliyopembuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake na kwamba, ni dhamana ya Mama Kanisa kuhakikisha kuwa anaendeleza mchakato wa Uinjilishaji mintarafu dini ya Kiyahudi. Tafakari hii ya kitaalimungu inalenga pamoja na mambo mengine kuwasaidia waamini wa dini hizi mbili kujenga na kudumisha uhusiano wa dhati mintarafu imani yao.

Ikumbukwe kwamba, Waraka huu si Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki, bali tafakari ya kina iliyofanywa na Tume ya Kipapa ya Majadiliano ya kidini na Wayahudi kuhusu mambo msingi ya kitaalimungu yanayowagusa waamini kwa nyakati hizi tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Huu ni msingi wa majadiliano kati ya waamini wa dini hizi mbili na kwamba, Waraka huu una utajiri mkubwa unaoweza kuwasaidia waamini wa dini hizi mbili kitaalimungu, tayari kujikita katika majadiliano ya kidini.

Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita Waraka wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano ya kidini umepewa uzito wa pekee katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa na kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchakato wa majadiliano kati ya Wayahudi na Wakristo kwa kuimarisha urafiki kati ya waamini wa dini hizi mbili. Katika Waraka wa “Nostra aetate” Kanisa Katoliki lilionesha msimamo wake wa kitaalimungu mintarafu dini ya Kiyahudi.

Majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi yanatofautiana kabisa na majadiliano haya na dini nyingine duniani, hii inatokana na mzizi unaowafungamanisha waamini wa dini hizi mbili. Yesu anaweza kufahamika vyema zaidi ikiwa kama ataangaliwa kadiri ya mazingira ya Kiyahudi kwa wakati wake, hata kama Yesu ni Masiha wa Waisraeli na Mwana wa Mungu anavuka mipaka ya uelewa huo wa kihistoria. Mwenyezi Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu amejifunua kama “Neno wa Mungu” akapata nafasi ya kukutana na watu. Neno la Mungu kwa Wayahudi linafahamika kama “Torah”; kwa Wakristo Neno la Mungu limemwilishwa katika Kristo Yesu na haligawanyiki hata kidogo na kwamba, linawataka waamini wa dini hizi mbili kutoa majibu muafaka ili kudumisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu.

Waraka huu unaendelea kukazia kwamba, Agano la Kale na Agano Jipya limeunganika na kushikamana kwa dhati hata kama tafsiri yake ina tofautiana kutokana na Mapokeo ya waamini wa dini hizi mbili. Kwa wakristo Agano la Kale pinapata utimilifu wake kwenye Agano Jipya na kwamba, Maagano yote mawili yanajenga historia ya Agano kati ya Mungu na watu wake na kwamba, Agano Jipya linapaswa kuchukuliwa kama utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Agano la Kale.

Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, watu wote wanashirikishwa kazi ya ukombozi na kwamba, wote wamekombolewa. Hata kama Wayahudi hawaamini kwamba, Yesu Kristo ndiye Mkombozi wa dunia, lakini wao pia wanahesabiwa kuwa ni sehemu ya wokovu huu kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake.(Rej. Rom. 11: 29). Kile kinachofanyika kwa sasa kinaendelea kubaki kuwa sehemu ya Fumbo la kazi ya Ukombozi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hata pale Wakristo wakati wa majadiliano ya kidini na Wayahudi wanaposhuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, hawana sababu ya msingi ya kutaka kuwaongoa Wayahudi. Kanisa linakaza kusema, halina madaraka wala utume unaoelekezwa kwa Wayahudi. Katika mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakristo, wanapaswa kufahamiana zaidi; kujipatanisha na kushikamana ili kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kupinga aina zote za ukatili dhidi ya Wayahudi. Wakristo na Wayahudi wanapaswa kweli kushirikiana katika utoaji wa huduma za kibinadamu kwa ajili ya kuwaendeleza maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wote kwa pamoja waweze kuwa ni kielelezo cha baraka kwa walimwengu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.