2015-12-10 11:57:00

Mwachieni Mungu nafasi ili aweze kuwafariji kwa huruma yake!


Mwenyezi Mungu anaupenda unyenyekevu wa binadamu na kwamba huruma yake haina mipaka. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 10 Desemba 2015; Ibada ambayo imehudhuriwa pia na wajumbe wa Baraza la Makardinali washauri ambao wameanza mkutano wao wa kumi na mbili hapa mjini Vatican na unahudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake ni sawa na Baba mwenye huruma anayependa kuwabembeleza watoto wake wadogo, ili aweze kuwahakikishia usalama wa maisha yao. Mwenyezi Mungu anatambua kwamba, amechagua watu wake, anaowatambua kwa unyonge na umaskini wao, lakini Yeye ni mwingi wa huruma na mapendo. Mwenyezi Mungu anawapenda watu wake upeo kama wazazi wanavyowapenda na kuwajali watoto wao, ili kuwahakikishia usalama wa maisha. Mungu anatambua udhaifu na dhambi za watu wake, anataka watubu na kumwongokea, ili aweze kuwaonjesha huruma na msamaha wake.

Huyu ndiye Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mwenyezi Mungu anawataka waja wake kufanya toba zaidi ili wapate ondoleo la dhambi, kwani anataka kujitwika udhaifu wa binadamu, dhambi na mapungufu yao, ili apate kuwapumzisha kama anavyosema katika Maandiko Matakatifu, njooni kwangu ninyi nyote mnaosumbuka na kuelemewa na mizigo nami nitawapumzisha, kwa kuwaondolea dhambi na kuwajalia amani na utulivu wa ndani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi ndivyo ambavyo Mwenyezi Mungu anavyowakirimia watu wake huruma na mapendo, ili nao waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma yake kwa watu wanaowazunguka. Mwenyezi Mungu ni mpole hata pale mwanadamu anapotenda dhambi kubwa, anapojikatia tamaa na kupoteza dira na mwelekeo wa maisha, lakini Mungu bado anamkirimia nafasi ya kutubu na kuongoka, ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie tena ile neema ya kuamsha ndani mwao imani inayojikita katika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, ili wao pia waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.