2015-12-10 08:32:00

Jubilei ya huruma ya Mungu: Kipaumbele ni kwa maskini!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi muafaka cha toba na wongofu wa ndani, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuambata upendo unaomwilishwa katika upendeleo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii inatokana na ukweli kwamba, ulimwengu mamboleo unaendelea kushuhudia vita, kinzani, migogoro na maafa, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuambata huruma na upatanisho unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa watu kuishi kama ndugu huku wakishirikishana haki, amani na mapendo kamili kama tiba muafaka ya kuganga na kuponya majeraha yanayomwandama mwanadamu!

Hii ni changamoto endelevu inayotolewa na Monsinyo Olivier Michel Marie Schmitthaeusler, msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki la Phnom-Penh, lililoko nchini Cambodia katika Waraka wake wa kichungaji wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Waamini wanahimizwa kuingia katika lango la huruma ya Mungu, ambalo ni Kristo Yesu. Katika maadhimisho haya, waamini pia watapata nafasi ya kushuhudia onesho la Mashuhuda wa imani kutoka nchini Cambodia walioyamimina maisha yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kufanya hija za maisha ya kiroho, ili kujipatia rehena na neema zinazotolewa na Mama Kanisa katika kipindi kama hiki kwa kutimiza masharti yanayotolewa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuambata rehema na neema zinazobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Ni wakati wa kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili kwa wahitaji, lakini upendeleo wa pekee wapewe maskini, ili nao waweze kuonja huruma hii kutoka kwa waja wake. Hili ni kundi kubwa katika Jamii ya wananchi wa Cambodia. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni chemchemi ya faraja na mapendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.