2015-12-09 10:07:00

watu wote waguswe na huruma na upendo wa Mungu popote pale walipo!


Baba Mtakatifu Francisko alianza kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu wakati hija yake ya kitume Barani Afrika, alipofungua Lango kuu la Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Bangui; mji ambao uko pembezoni mwa Jumuiya ya Kimataifa kwa siku moja, ukawa ni mji wa sala kwa ajili ya kuombea haki, amani, upatanisho na mwaliko kwa waamini kupia Lango la huruma ya Mungu, kwa kuachana na ukale wa maisha, ili kuambata rehema na neema inayotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu katika maisha yao!

Wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, Baba Mtakatifu alizundua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kufungua Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 8 Desemba 2015. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kupitia Lango la huruma ya Mungu kwa kuachana na dhambi, ili kuambata huruma ya Mungu inayowasindikiza daima katika hija ya maisha yao hapa duniani, hadi siku ile watakapokutana na Muumba wao, Hakimu mwenye haki! Ushuhuda wa waamini ni muhimu sana katika maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu ili uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani toba na wongofu wa ndani!

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anakaza kusema, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio, asubuhi majira ya Saa: 3:30 kwa saa za Ulaya, tarehe 13 Desemba 2015, Baba Mtakatifu Francisko atafungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma na baadaye Malango ya Makanisa makuu ya Kipapa yaliyoko hapa mjini Roma yatafunguliwa na tukio hili litafanyika pia kwenye Makanisa makuu sehemu mbali mbali za dunia.

Malango ya Madhabahu na Makanisa makuu yatakuwa wazi katika kipindi cha Mwaka mzima wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kujipatia neema na rehema zinazotolewa na Mama Kanisa katika Mwaka huu mtakatifu, tayari kuambata toba na wongofu wa ndani, ili kupyaisha maisha ya kiroho yanayoshuhudiwa kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni ishara wazi ya umoja na mshikamano wa Kanisa chini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia.

Baba Mtakatifu ataanza Ibada kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, huku mkononi akiwa amebeba Injili na baadaye, atafuatiwa na Kardinali Agostino Vallini na Maaskofu wasaidizi wa Jimbo kuu la Roma, Mapadre wahudumu wa maisha ya Kiroho Kanisa hapo. Watafuatia Wakleri, Watawa na Waamini walei walioteuliwa kuwawakilisha walei wenzao. Kwa pamoja watafanya maandamano kuelekea kwenye Altare kuu na badaye itaendelea Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio. Mapadre wote wa Jimbo kuu la Roma watashiriki katika Ibada hii.

Itakumbukwa kwamba, Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kwa mara ya kwanza lilifunguliwa kunako mwaka 1423 na Papa Martin wa V wakati wa maadhimisho ya Jubilei. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu anataka watu wote walau waweze kuguswa na huruma ya Mungu popote pale walipo, kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu yuko daima na watu wake. Kumbe, juhudi za makusudi kabisa hazina budi kufanywa ili lengo hili liweze kufikiwa kwa sehemu kubwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.