2015-12-09 08:23:00

Papa amwelezea Bikira Maria mateso, mahangaiko na matumaini ya watu wake!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Desemba 2015 baada ya kuzindua Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jioni alikwenda kutoa heshima zake za dhati kwa ajili yake na kwa niaba ya Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma kwa Sanamu ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili iliyoko kwenye Uwanja wa Spagna, kati kati ya Jiji la Roma na hapo akakutana na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema waliofurika ili kusali pamoja naye!

Utamaduni wa kutoa heshima kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili unapata chimbuko lake kunako tarehe 8 Desemba 1854 Papa Pio IX alipotangaza kwamba, Bikira Maria tangu nukta ya kutungwa kwake mimba kwa neema na upendeleo wa Mwenyezi, kwa kutazamia mastahili ya Yesu Kristo, Mwokozi wa wanadamu wote alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Miaka mitatu baadaye, kunako mwaka 1857, Papa Pio IX akazindua mnara wa Sanamu ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili.

Tangu wakati huo, Mapapa wamekuwa wakitoa heshima zao kwa Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili kwa kuweka shada la maua kwenye mnara wa Sanamu hii. Kwa namna ya pekee, Mwenyeheri Paulo VI mara baada ya kuhitimisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, tarehe 8 Desemba 1965 alikwenda kumshukuru Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili kwa kufanikisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Imepita miaka hamsini tangu tukio hili la kihistoria lilipotokea.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anatapenda kulielekeza Kanisa katika hija ya huruma ya Mungu kwa kuamsha tena ari na mwamko wa kimissionari kama ilivyokuwa wakati wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu akiwa chini ya Sanamu ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili amemtolea sala ya heshima, imani na mapendo kwa Mama wa huruma ya Mungu akiiweka Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma chini ya ulinzi na tunza ya Mama wa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawaweka watoto, vijana, wazee, wagonjwa, wafungwa na wale wote wanaojisikia kuelemewa na mzigo wa safari ya maisha chini ya Bikira Maria Mama wa huruma ya Mungu, bila kuwasahau wahamiaji na wakimbizi wanaotoka mbali wakitafuta amani na fursa za kazi. Baba Mtakatifu anawaweka wote hawa chini ya ulinzi wa Bikira Maria kwani katika ulinzi na tunza yake, wote wanapata nafasi ya kuonja upendo wa Mungu ambao kwa namna ya pekee unajionesha kwa njia ya Kristo Yesu aliyefanyika mwili na kuwa ni ndugu na Mkombozi wa binadamu wote.

Baba Mtakatifu anaendelea kusali kwa kusema kwamba, kwa njia ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili, Kanisa linatambua ushindi wa huruma ya Mungu dhidi ya dhambi na matokeo yake na hivyo anaamsha ndani ya waamini matumaini ya maisha bora zaidi ambayo hayafungwi na utumwa wa dhambi, masikitiko wala woga. Chini ya miguu ya Bikira Maria waamini wanasikia tena ile sauti ya mwaliko wa kuanza hija ya kuelekea kwenye Lango linalomwakilisha Yesu Kristo, kwa imani na matumaini ili waweze kukirimiwa zawadi ya huruma. Waamini wasiogope wala kuona aibu kwani Mwenyezi Mungu anawasubiri ili kuwapokea na kuwakaribisha nyumbani mwake, ili waweze kufarijika kutoka kwenye chemchemi ya amani na furaha. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili kwani kwa njia ya safari hii ya upatanisho yuko karibu na watoto wake na anaendelea kuwasindikiza na kuwaenzi hata katika magumu yao!

Baba Mtakatifu mara baada ya sala hii kwa Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili, alisalimiana na wagonjwa na wazee waliokuwa wamemiminika kwenye Uwanja wa Spagna, ili kusali pamoja na Baba Mtakatifu kwa kumshukuru Mungu kwa kuzindua Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto ya kuambata toba na wongofu wa ndani, ili kutembea katika hija ya huruma na upendo wa Mungu pamoja na kushuhudia huruma hii kwa njia ya matendo ya huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.