2015-12-09 09:55:00

Huruma ya Mungu ni kiini cha Injili!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuzindua rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 9 Desemba 2015 amefafanua kuhusu umuhimu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwani inajikita katika mambo msingi ya Injili, changamoto na mwaliko kwa waamini pamoja nawatu wote wenye mapenzi mema kumwilisha huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwa kuishi kadiri anavyotaka Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kumekuwepo na mabadiliko makubwa duniani na kwamba, Mama Kanisa kwa namna ya pekee anahamasishwa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu inayoweza kushinda dhambi za binadamu na hatimaye, kumpatia mwanadamu uhuru kamili! Huruma ya Mungu inajionesha miongoni mwa watu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu ambaye ni kiini cha Injili. Maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu ni kielelezo cha kile ambacho Mwenyezi Mungu anapendelea zaidi katika maisha; mambo msingi yanayopaswa kumwilishwa katika maisha, utume na miundo mbinu ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, leo hii huruma na msamaha ni maneno ambayo yanaonekana kumezwa zaidi na ubinafsi; raha na starehe na katika maisha ya Wakristo maneno haya yanachafuliwa na unafiki pamoja na kupenda kumezwa zaidi na malimwengu. Kwa kusahau huruma ya Mungu katika maisha, anasema Baba Mtakatifu, mwamini anashindwa kuona na kutambua dhambi katika maisha yake. Mambo haya yanaonesha umuhimu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu inayopaswa kumwandama mwanadamu katika hija yake ya maisha.

Baba Mtakatifu anahitimisha Katekesi yake kuhusu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuwataka waamini kumwomba Kristo Yesu ili awasaidie kutambua zaidi na zaidi uwepo wa huruma ya Mungu inayotenda kazi katika maisha yao; tayari kuishuhudia kama chachu ya nguvu kubwa inayoleta mabadiliko ulimwenguni. Bikira Maria ni Mama wa Huruma ya Mungu ambaye ameukirimia ulimwengu zawadi ya Kristo Yesu, chemchemi ya huruma ya Mungu. Bikira Maria awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukutana na Yesu Kristo mwingi wa huruma na mapendo, ili wao pia waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutoka Mashariki ya Kati kuhakikisha kwamba, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu unawasaidia kuonja msamaha, tayari kupokea na kutoa msamaha kwa wale waote wanaokutana nao katika safari ya maisha yao,  ili kushuhudia huruma ya Mungu katika dunia hii ambayo kwa wakati huu inaonekana kuwa kama uwanja wa fujo! Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni changamoto ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha, ili kuwa wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Waamini wawe wepesi kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili katika maisha yao kwa kutenda kadiri anavyotaka Mwenyezi Mungu. Vijana wawe tayari kumpokea Masiha anayezaliwa kwa mara nyingine tena mioyoni mwao; wagonjwa wapokee na kuambata neema ya Mungu katika maisha yao na kwamba, huruma iwe ni kiini na dira ya maisha ya wanandoa wapya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.