2015-12-08 15:20:00

Yesu Kristo ndiye mlango wa maisha ya uzima wa milele!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Desemba 2015 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na mara baada ya Misa, amefungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ishara ya Kristo aliye njia, ukweli na uzima, changamoto na mwaliko kwa waamini kuvua utu wao wa kale, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Ibada ya Misa takatifu imetanguliwa na tafakari zilizochotwa kutoka katika Matamko makuu ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: Neno la Mungu, Dei Verbum, Fumbo la Kanisa, Lumen Gentium; Liturujia ya Kanisa Sacrosantum concilium, Kanisa na Ulimwengu, Gaudium et spes.

Waamini wamesikiliza pia sehemu ya nyaraka kuhusu Majadiliano ya Kiekumene: Unitatis redientegrazio pamoja na Uhuru wa kidini, Dignitatis humanae. Nyaraka hizi ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu amesali kabla ya kufungua Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Amewakumbusha waamini kwamba, Kristo ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kukumbatia toba, wongofu na utakatifu wa maisha. Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha na amani ya ndani. Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki.

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa wa kwanza kuvuka Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, akaingia na kusali kwa kitambo kidogo, akafuatiwa na Papa Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, baadaye  yakafuata maandamano ya Wakleri, Watawa na Waamini walei waliokuwa wameteuliwa rasmi kwa ajili ya tukio hili! Ukaimbwa wimbo maalum wa Jubilei ya huruma ya Mungu ambao kwa sasa tayari umekwisha tafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na kutungiwa maneno.

Baada ya kuzunguka kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko alitoa baraka zake na huo ukawa ni mwisho wa Ibada ya Misa Takatifu katika Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili sanjari na uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na ufunguzi wa Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.