2015-12-08 08:34:00

Jubilei ya huruma ya Mungu ni tukio la Watu wa Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro huruma ya Mungu na msamaha ni maneno ambayo yameongoza maisha na utume wake hadi wakati huu. Ilikuwa ni tarehe 29 Agosti 2014 kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu Francisko alianza kugusia umuhimu wa Kanisa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo kamwe haachi kuwasamehe watoto wake wanaomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata huruma na msamaha wake, kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma anayesimuliwa na Mwinjili Luka!

Hii ni tafakari inayotolewa na Askofu mkuu Rino Fisichella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya, Baraza ambalo limepewa dhamana ya kuratibu na kusimamia maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Maadhimisho haya ni mwaliko kwa waamini kukimbilia na kufumbata huruma ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu alizindua maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati, wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika. Siku hiyo, Bangui ukawa ni mji mkuu wa sala na Madhabahu ya kuombea huruma na upatanisho kati ya watu.

Baba Mtakatifu alitoa kipaumbele cha kwanza kwa huruma ya Mungu wakati wa hija yake Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, akawataka wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, msamaha , huruma na upatanisho; mambo makuu yanayotiliwa mkazo na Mama Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu. Wananchi wa Afrika ya Kati, wawe tayari kuvuka na kuanza maisha mapya yanyomwambata Kristo, tayari kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa amani na upatanisho unaobubujika kutoka katika undani wa maisha yao.

Askofu mkuu Fisichella anasema, maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu yanajikita katika uhalisia wa maisha ndiyo maana kauli mbiu ya maadhimisho haya inasema “Iweni na huruma kama Baba Yenu”. Hapa waamini wanapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima yu karibu nao na kwamba, hata wao wanahamasishwa kuwa kweli ni vyombo vya huruma ya Mungu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa linapaswa kuwa ni sauti ya kinabii na sauti ya wanyonge. Kanisa liwe tayari kuganga na kuponya madonda ya utengano kwa njia ya huruma, upendo na mshikamano wa dhati.

Watu waguswe na mahangaiko pamoja na mateso ya jirani zao kwa kufungua macho na masikio, tayari kujibu kilio cha damu! Waamini wanahamasishwa kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika walio uchi; kuwakaribisha wageni; kuwaponya wagonjwa, kuwatembelea wafungwa na kuzika wafu! Matendo ya huruma kiroho yanajikita katika ushauri kwa walio mashakani; kuwafunza wajinga; kuwaonya wadhambi; kuwafariji waliojeruhiwa; Kusamahe maovu; kuchukuliana kwa saburi na wale wanaowatendea wengine maovu pamoja na kuwaombea walio hai na wafu! Ikumbukwe kwamba, matendo ya huruma ni kipimo cha kuingia katika maisha ya uzima wa milele na kwamba, waamini wanatumwa kuwatangazia jirani zao Injili ya huruma ya Mungu!

Askofu mkuu Fisichella anasema haya ni matendo ya kawaida yanayoweza kutekelezwa na kila mwamini kadiri ya uwezo wake, lakini yana maana sana katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawakumbuka wafungwa ambao wanaendelea kutumikia vifungo katika magereza mbali mbali. Hata wao wanaweza kuuvua utu wa kale na kujivika utu mpya kwa njia ya toba na wongofu wa ndani pamoja na kupania kuyaacha maisha yao yaliyochakaa kwa dhambi, ili kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Wafungwa wawe na ujasiri wa kuingia katika lango la huruma ya Mungu.

Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ndiyo walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu anatarajiwa kufungua mlango wa huduma kwa maskini inayotolewa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Italia. Hapa ni mahali pa ukarimu kwa wenye njaa na kiu; mwaliko kwa Makanisa mahalia pia kuwa na vituo maalum kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Askofu mkuu Fisichella anasema katika ulimwengu wa utandawazi ambamo kumejaa wasi wasi na hofu kuhusu vitendo vya kigaidi na ukosefu wa ulinzi na usalama, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kwanza kabisa kufungua malango ya mioyo yao, tayari kumkaribisha Kristo anayetaka kufanya makazi pamoja nao! Waamini wawe na ujasiri wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini yanayojikita katika ukweli na uwazi, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kutoa ulinzi madhubuti kwa raia na mali zao kwa kuheshimu uhuru wa kuabudu, ustawi na maendeleo ya wengi.

Waamini wa dini mbali mbali katika maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu wajitaabishe kufahamiana, kuheshimiana na kuthaminiana na kwamba, tofauti zao za kidini na kiimani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, zawadi ambayo inapaswa kuendelezwa! Ikumbukwe kwamba, Jubilei ya huruma ya Mungu ni tukio la maisha ya kiroho linalogusa watu katika undani wa maisha yao. Ni hija ya Mama Kanisa anayetaka kupyaisha maisha ya watoto wake kwa kuuvua utu wa kale, tayari kumwambata Kristo mwingi wa huruma na mapendo. Kanisa linapaswa kuwa ni chemchemi ya huruma na mapendo ya Mungu yanayoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha. Hii ndiyo changamoto kubwa inayowasubiri waamini wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anakaza kusema Askofu mkuu Rino Fisichella.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.