2015-12-08 15:29:00

Bikira Maria ni shuhuda wa upendo na huruma ya Mungu


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na ufunguzi wa Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumanne, tarehe 8 Desemba 2015, Baba Mtakatifu pia aliowaongoza waamini katika tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana kwa kuonesha upendeleo wa pekee ambao Bikira Maria alijaliwa na Mwenyezi Mungu kwa kumkinga na doa la dhambi ya asili. Licha ya dunia kutawaliwa na ubaya wa dhambi, lakini Bikira Maria hakuguswa hata kidogo na ubaya wa dhambi, kwani alikirimiwa neema hata kabla ya kutungwa mimba.

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili anasema baba Mtakatifu maana yake ni kwamba, Bikira Maria ni mwanadamu wa kwanza kabisa kukombolewa na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani, wokovu ambao Mwenyezi Mungu anataka kutoa zawadi kwa kila binadamu kwa njia ya Kristo Yesu. Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa kushinda dhambi! Kanisa linapoanza maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu linapenda kumwangalia Bikira Maria kama kielelezo cha upendo wenye imani, kwa kutafakari ukuu wake pamoja na kuiga imani aliyoishuhudia katika maisha yake, changamoto ya kuangalia mapambazuko ya dunia mpya, iliyobadilishwa kwa njia ya kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu; mapambazuko mapya yanayojikita katika huruma ya Mungu, kumbe, Bikira Maria ni Mama wa ubinadamu mpya!

Maadhimisho ya Siku kuu hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini kumwambata Mwenyezi Mungu na neema ya huruma yake katika maisha ya kila siku, ili kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa kufuata hija ya Kiinjili. Siku kuu hii inaweza kuwa ni kwa ajili ya wote, ikiwa kama watu wataweza kufisha ubinafsi wao, kwa kuwatangazia na kuwashuhudia wengine Injili ya furaha na matumaini pamoja na kuwashirikisha upendo usiokuwa na kifani, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, watu waliokuwa na upendeleo wa pekee machoni pa Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika umwilishaji wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili ni kumbu kumbu endelevu ya zawadi na huruma ya Mungu katika maisha ya waja wake. Bikira Maria alikuwa wa kwanza kukombolewa, mfano wa Kanisa, mchumba wa Kristo asiye kuwa na doa, anayependeka sana, awasaidie watoto wake kugundua huruma ya Mungu kama utambulisho wao wa maisha ya Kikristo yanayoonesha ile sura ya Kristo mwenyewe, tayari kukutana na wote, ili kuwaganga na kuwaponya waliopondeka na kuvunjika moyo; tayari kushirikiana na wadhambi, ili watubu na kumwongokea Mungu, tayari kuonja msamaha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, binafsi ana ibada kubwa kwa Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.