2015-12-07 07:32:00

Jumapili ya mshikamano na waamini wa Kanisa la Mashariki!


Heri wenye rehema maana hao watapata rehema ndiyo kauli mbiu inayoongoza Siku ya Sala kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, inayoadhimishwa tarehe 6 Desemba 2015, yaani Jumapili ya pili ya Kipindi cha Majilio nchini Poland. Kauli mbiu hii ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika uzinduzi na hatimaye, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu unaozinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2015.

Kauli mbiu hii pia ndiyo inayoongoza maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016 itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, Poland. Lengo la Baraza la Maaskofu Katoliki Poland ni kusaidia mchakato wa kuwajengea uwezo vijana maskini wanaoishi huko Mashariki, hususan katika nchi ambazo zilikuwa chini ya mfumo wa Kikomunisti, jukumu ambalo lilianzishwa kunako mwaka 1989. Jimbo kuu la Cracovia linatarajia kutoa malazi kwa vijana wengi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016.

Mwaka huu macho ya huruma kutoka Poland yanaelekezwa zaidi nchini Ukraine ambako bado mtutu wa bunduki unarindima. Huko kuna watu ambao wanaendelea kukosa mahitaji msingi. Mchango huu utasaidia kugharimia walau huduma msingi kwa vituo vya kulelea watoto wadogo, wazee na wanawake wanaolea watoto wao wenyewe bila msaada wa wenzi wao wa ndoa. Kunako mwaka 2014 jumla ya Euro 6,000 zilikusanywa kutoka kwa waamini ili kugharimia miradi 350 iliyokuwa imependekezwa. Katika kipindi cha miaka kumi na sita, kiasi cha Euro millioni kumi na tano zimekusanywa kutoka kwa waamini ili kusaidia nchi kama: Russia, Bielorussia, Kazakistan, Lithuania, Georgia na Serbia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.