2015-12-05 08:02:00

Papa Francisko amewakuna wengi Barani Afrika!


Kardinali Wilfrid Fox Napier wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini katika mahojiano maalum na Shirika la Habari za Kimissionari, FIDES anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake Barani Afrika kwa hakika amekuwa ni mjumbe wa Injili ya amani, matumaini na upatanisho na kwamba, sehemu kubwa ya ujumbe wake inagusa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Ujumbe wa Baba Mtakatifu nchini Kenya, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati ulikuwa ni matamanio makubwa ya Familia ya Mungu Barani Afrika.

Kardinali Napier anasema, Baba Mtakatifu amegusia kwa namna ya pekee umuhimu wa kuwa ni vyombo na wajenzi wa haki, amani na upatanisho, hii ni changamoto endelevu kwa nchi nyingi Barani Afrika. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa Barani Afrika katika maisha na utume wake kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma kwa maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Haya ni mambo msingi ambayo yamewagusa wengi si kwa maneno tu, bali kwa ushuhuda ambao umeoneshwa na Baba Mtakatifu mwenyewe!

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza sana Makatekista Barani Afrika kwa kutambua mchango na huduma yao kwa Kanisa Barani Afrika kwani wanafanya kazi takatifu ambayo kimsingi ndio utambulisho wao wanapoisaidia Familia ya Mungu katika malezi na majiundo ya: Imani, Sakramenti, Maisha adili na Sala. Makatekista wakiishi kiamimifu utume wao unaoambata Katekesi, waweza kuwa kweli ni mashuhuda na mfano bora wa kuigwa na wengi Barani Afrika. Makatekista wawe kweli ni mfano bora wa imani inayomwilishwa katika matendo!

Kardinali Napier anakiri kwamba, Afrika ya Kusini kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo pengine ni wasi wasi usiokuwa na mashiko wala mvuto dhidi ya wahamiaji wanaotafuta riziki ya maisha nchini humo. Kwa bahati mbaya wananchi wengi wa Afrika ya Kusini wamesahau ukarimu, upendo na mshikamano waliooneshwa na nchi kadhaa za Kiafrika walipokuwa bado chini ya utawala wa Serikali ya ubaguzi wa rangi. Matukio ya ukatili dhidi ya wahamiaji na wakimbizi wanaoishi Afrika ya Kusini yamefunikwa tu, lakini bado hayajapatiwa ufumbuzi wa kudumu, iko siku yatalipuka na kusababisha tena majanga.

Kardinali Napier anasema, shida ni umaskini na hali ngumu ya maisha unaotokana na ukosefu wa fursa za ajira pamoja na hali ngumu ya uchumi. Mashambulizi haya yanafanywa katika misingi ya kibaguzi kwa kudhani kwamba, waafrika wenzao ndio chanzo cha hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo! Si rahisi sana kusikia kwamba, makundi ya vijana yamewashambulia wafanyabiashara kutoka Asia, Pakistan au katika nchi yoyote ya Ulaya, lakini mashambulizi haya yanaelekezwa kwa Waafrika wenzao! Aibu ya mwaka!

Kardinali Wilfrid Fox Napier anahitimisha mahojiano haya kwa kusema, Bara la Afrika limebahatika kuwa na rasilimali watu na maliasili; ambayo ikitumika vyema  kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, umaskini, njaa, ujinga na maradhi ni mambo yanayoweza kupewa kisogo. Kuna haja kwa viongozi wa Serikali kupambana na rushwa pamoja na ufisadi wa mali ya umma, mambo ambayo yanakwamisha mchakato wa haki, amani na maendeleo ya nchi. Umefika wakati kwa viongozi wa Serikali na Kidini pamoja na wananchi wote kwa ujumla wao kujikita katika maadili na utu wema; kwa kumtanguliza kwanza Mwenyezi Mungu na kuwaheshimu wananchi wenzao.

Viongozi wawe ni mfano wa uaminifu na uadilifu, tayari kujisadaka na kuwajibika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi badala ya kutawaliwa na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka, mambo ambayo matokeo yake ni vita, kinzani na mipasuko ya kijamii! Kanisa linalo mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.