2015-12-05 08:43:00

Mbele ya ukubwa wa dhambi, Mungu anajibu kwa huruma na mapendo kamili!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Desemba 2015 majira ya saa 3:30 asubuhi anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na kufungua lango kuu la Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu sanjari na Siku kuu ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili. Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria alipata upendeleo wa pekee kwa kuwa ni Mama wa mkombozi kwa kutungwa mimba pasi na dhambi ya asili ili aweze kumzaa Mwana wa Baba wa milele.

Mbele ya ukubwa wa dhambi, Mwenyezi Mungu anajibu kwa njia ya msamaha kamili hapa Mwenyezi Mungu anataka kuonesha ukuu wa msamaha katika maisha ya waja wake. Ufunguzi wa lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ni mwaliko wa kuingia katika lango la huruma, ambamo waamini wataonja mapendo ya Mungu anayefariji, anayesamehe na anayewapatia watu wake matumaini mapya. Siku kuu hii pia ina umuhimu wake katika historia, maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi.

Ni kumbu kumbu ya Maadhimisho ya kuhitimishwa kwa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani; tayari kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili katika mwelekeo mpya, kwa kuwa ni mashuhuda wa imani na ujasiri unaoambata neema na rehema ya Mungu, ili kuwamegea walimwengu huruma na upendo wa Mungu Baba! Ni wakati wa kumwilisha huruma zaidi kuliko ukali; kushuhudia upendo wa kimama, uvumilivu na mapendo hata kwa wale waliojitenga na Kanisa, kielelezo cha Kristo Msamaria mwema.

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni chemchemi ya Injili ya matumaini badala ya woga na hali za kutisha na kukatisha tamaa. Lengo la Mababa wa Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican ni kumheshimu Mungu na kumhudumia vyema mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hata katika mapungufu yake. Baba Mtakatifu anataka kuwaingiza waamini katika Lango takatifu kwa imani na matumaini, ili kuambata nguvu ya Kristo Mfufuka; Roho Mtakatifu anayewaongoza waamini kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, ili wote kwa pamoja waweze kuuna uso wa huruma ya Mungu.

Hizi ndizo sababu msingi zilizomfanya Baba Mtakatifu Francisko licha ya kuwa na Ibada ya pekee kabisa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa lakini kuna sababu pia za kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa ambazo, Baba Mtakatifu ametaka kuzizingatia katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.