2015-12-05 16:03:00

Kanisa linasherehekea ushindi dhidi ya gonjwa hatari kabisa!


Ndugu zangu, hapa duniani yako magonjwa mbalimbali anayoweza kuugua binadamu kama vile kichwa, macho, masikio, tumbo, moyo, mapafu, figo, na mengine ya hatari kama, Saratani, Ukimwi, Ebola pengine hata Kipindupindu nk. Leo tutaliona gonjwa ambalo kila mmoja amezaliwa nalo na anatembea nalo na anakufa nalo. Gonjwa hilo ni sugu na linanyonya kinga zote za mwili, za akili hata kiroho na kumdhoofisha mtu kiasi cha kuingiliwa kirahisi na magonjwa mengine yote unayoweza kuyafikiria. Jambo la kushangaza ni kwamba kuna binadamu mmoja tu aliyebahatika kutoathirika na gonjwa hilo. Gonjwa hilo utaligundua kwenye tamko lifuatalo: “Mwenye heri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mungu Mwenyezi; kwa kutazamia mastahili ya yesu Kristo Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya.” Tamko hili lilitolewa na Papa Pio IX kunako mwaka 1854.

Wataalamu wengi wametafakari kwa kina maana na chanzo cha “dhambi ya asili.” Mtakatifu Augustin na wataalamu wengine walieleza kuwa chanzo cha dhambi ya asili ni wazee wetu Adamu na Eva walikosa kutomtii Mungu. Kabla yake walishirikiana vizuri kati yao wao na viumbe wengine, na kila mmoja alijisikia kuwa ni zawadi kwa mwingine. Walihusiana vyema na muumbaji wao, wakifuata sera zake. Lakini kadiri ya utafiti yasemwa kwamba kati ya viumbe aliibuka shetani aliyezua tafulani kwa kumshawishi binadamu kuachana na sera za Mungu. Ingawaje ukisoma kwa makini Agano la Kale shetani hatamkwi kabisa badala yake anatajwa nyoka. Kwamba kutokana na ujanja wake akamrubuni Adam na Eva ili kumkaidi Mungu. Basi Mungu akatoa adhabu kwa wazee wetu iliyotuathiri hadi sisi watoto wao.

Tamko jingine la dhambi ya asili linaloendelea kutuzuga hadi leo ni pale linaposema kuwa Maria peke yake ndiye aliyekingwa dhambi hiyo ya asili. Endapo Mungu ni Baba yetu sote, kulikoni atoe fursa kwa binadamu mmoja wakati dhambi imetuthiri sisi sote. Wanataalimungu wa Maandiko Matakatifu wametafakari utata huo na kuona kuwa tamko hilo la kukingwa dhambi ya asili halitokani na tafakari ya kibiblia, bali ni tafakari ya mashabiki waliokuwa na mapenzi ya pekee kwa Mama Bikira Maria. Kwa hiyo si ajabu pia kuona kwamba tamko hilo limesababisha sintofahamu ndani ya ukristo. Ili kuepuka sintofahamu hiyo hatuna budi kulitafakari tamko hilo kwa mtazamo wa biblia. Wanataalimungu wameitafakari Biblia na kuona kwamba dhambi ya asili haitokani na Adamu na Eva.

Lengo la Biblia katika simulizi hili lilitokana na  tafakari ya swali kuu lililokuwa kiini cha moyo wa binadamu na kujaribu kulipatia jibu. Swali hilo lilitokana na hali halisi iliyoiathiri duniani. Ulimwengu ulikuwa umekithiri kwa vitendo viovu vya mauaji, madhulumu, njaa, kiu, magonjwa, vilio. Dunia ikaonekana kuwa kama bonde la machozi.  Ndipo lilipoibuka swali: “Nini ni kisa cha mikasa hiyo yote.” Swali hilo limeendelea kuulizwa na binadamu daima hadi leo. Basi wanatauhidi hao wakaanza kumtafuta mchawi kati ya Mungu na binadamu.

Kwa vyovyote kutokana na Biblia msababishaji siyo Mungu, kwani inatueleza waziwazi kwamba Mungu ni upendo, na ametuumba kwa mfano wa sura yake ya upendo. Baada ya uumbaji akaona kila kitu ni chema. Akatengeneza bustani ya Paradisi na kumweka binadamu na kumtakia kuishi kwa upendo humo bustanini. Kinyume chake Biblia inaeleza kwamba binadamu kwa makusudi mazima alikataa kufuata sera za Mungu, akaamua kufuata kichwa chake na kufanya mambo kivyake. Hali hiyo ilimfikisha pabaya hadi kujisikia amevuliwa nguo na kuanza kulia na kusaga meno.

Hali ya kutaka kuwa huru na kufuata kichwa chako unaiona hata leo katika maisha ya binadamu. Watu wanatumia uhuru wao katika mapenzi, katika kubugia unga, katika kunywa, katika kazi bila kumjali Mungu na kujali haki za wengine. Hawajui kwamba ukimwacha Mungu unakuwa mtupu. Mapato yake wanaishia kwenye bonde la machozi. Ama kweli “mtoto akililia wembe mpe.”  Mapato ya kumwacha Mungu, unaishia kumkana hata ndugu yako na kutumia kila alichoomba Mungu kwa ubinafsi. Hali hiyo unaiona pale Mungu alipomwuliza Adamu: “Labda umekula tunda la mti nililowakataza?” Adamu haoni kigagasi kumsaliti mke wake: “mwanamke uliyenipa ndiye alinidanganya.” Hivi ndivyo anavyofanya binadamu hadi leo pale mambo yanapomwendea vibaya, anamlaumu Mungu, na ndugu zake, nk.

Kadhalika mwanamke, anamtupia lawama nyoka ingawaje kwa kweli anataka kumlaumu Mungu mwenyewe. Hivi ndivyo afanyavyo kila binadamu anapotatika katika matatizo aliyojisababishia mwenyewe kwa ubinafsi wake. Tunamlaumu Mungu kwa kuumba ulimwengu ovyo, tunalaumu mfumo wa elimu, tunailaumu jamii, tunalaumu utawala, nk. kumbe ni msababishaji ni sisi wenyewe.  Mungu anaamua kutoa adhabu kwa Adam na Eva lakini nyoka anampa laana. “Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote.” (Mwanzo 3:14).  Laana maana yake ni utasa au kukosa uzao. Hiyo inaonesha kuwa ushetani, uovu na ubaya wote hautaendelea kuzaliana, bali utakomeshwa na upendo utatawala. Hatimaye tumegundua kwamba Joka ndiye aliyetema sumu kali inayotusababisha gonjwa wa ubinafsi.

Ndugu zangu kama tulivyona kwamba gonjwa hilo ubinafsi ni “kizaliwa nacho.” Kwa hiyo ubinafsi huo ni mimi mwenyewe. Binadamu tumeshaathirika na sumu hiyo ya nyoka tangu kuzaliwa na hakuna mtu aliyefaulu kujitibu kwa nguvu zake mwenyewe. Kwa hiyo tunahitaji kinga toka kwa Mungu mwenyewe. Nguvu ya kinga hiyo itatusaidia kufubaza makali ya sumu hiyo. Tunatulizwa na maneno ya Paulo aliyowaandikia Waefeso kwamba “Katika Kristo, Mungu alituchagua kabla ya kuumbwa ulimwengu, ili kuwa watakatifu na bila doa mbele yake katika upendo kama watoto warithi wa Mungu” (Waef. 1:4) Hapa Paulo anatukumbusha asili yetu kuwa kila mmoja wetu aliumbwa vizuri. Kwamba Mungu alishatutenga kuwa watakatifu na safi bila doa – yaani imakulata, ila baadaye tumeathirika na sumu ya ubinafsi. Ili kufuta makali ya gonjwa hilo yatubidi kufuata ushauri nasaa yaani kumeza vidonge vya upendo wa Kristo.

Kadhalika kwa vile kinga ya sumu hiyo inatoka kwa Mungu, basi kuna binadamu mmoja aliyebahatika kukingwa nayo. Binadamu huyo ni Bikia Maria tunayemsherekea Sikukuu ya leo. Yeye peke yake hakuwa na ubinafsi, bali upendo kamili. Maisha yake yote yalikuwa ni zawadi ya upendo kwa Mungu. Ukweli huo hauna maana kwamba Maria hakujaribiwa, au hakuwa na matatizo yoyote katika maisha, la hasha bali aliyapata tena majaribu mengi sana. Lakini hakukubaliana na udanganyifu wa nyoka yule mjanja aliyejaa sumu ya ubinafsi. Bikira Maria pekee yake alifanikiwa kukanyaga kichwa cha nyoka yaani kuushinda ubinafsi. Daima Bikira Maria alimtii Mungu katika upendo. Maria ni kipeo cha mwito wetu wa kuwa watakatifu bila doa katika upendo kama watoto warithi wa Mungu.” Heri sana kwa Sikukuu ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili na mwanzo wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, mwaliko na changamoto ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, tayari kuushuhudia kwa Watu wa Mataifa!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.