2015-12-04 10:19:00

Mkichezea fedha ya Magufuli kwenye huduma za kijamii mtakiona cha moto!


Serikali ya Tanzania imesaini mikataba miwili na Serikali ya Uswisi ili kuendeleza na kuimarisha huduma za kijamii nchini Tanzania hasa katika Sekta ya Afya. Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa tarehe 4 Desemba 2015 Jijini Dar es Salam Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile amesema kuwa kupitia ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili, Serikali ya Uswisi inaendelea kusaidia kuboresha Sekta ya Afya nchini hususani kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.  “Uswisi imesaidia Sekta ya Afya kwa miaka 15 na mpaka sasa imeshachangia jumla ya shilingi billion 181.7 tangu miradi ya afya ianzishwe nchini” alisema Likwelile.

Aidha, Dkt. Likwelile aliongeza kuwa Serikali ya Uswisi imelenga pia kusaidia kuimarisha utoaji wa huduma katika idara ya Afya katika Serikali za Mitaa kwa kuzingatia usawa na ubora wa huduma hizo hasa kwa wanawake,watoto pamoja na makundi yaliyotengwa hasa maeneo ya vijijini.  Zaidi ya hayo, Dkt. Likwelile amesema kuwa Serikali ya Uswisi itarajia kuungana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha sera za malipo kwa wafanyakazi wa Afya ili watoe huduma bora yenye tija kwa jamii.

Kwa upande wake Balozi wa Uswisi Nchini Tanzania Bi. Florence Tinguely Mattli amesema kuwa amefurahishwa na utoaji bora wa huduma za Afya Nchini Tanzania ambazo zimekuwa zenye tija kwa wananchi wanapokuwa wanahitaji huduma hizo kwa wakati. Bi. Florence aliongeza kuwa Serikali ya Uswisi kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya mkoa wa Dodoma umekuwa wa kwanza kunufaika na mfuko huo ambapo mikoa mingine inayotarajiwa kunufaika ni pamoja na Morogoro na Shinyanga ili kuboresha afya ya wanawake, watoto, vijana wazee na watu wasiojiweza.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Donan Mmbando alisema kuwa lengo la fedha hizo ni kuhakikisha huduma za Afya zinawafikia watu wote wenye mahitaji hayo kwa wakati. “Mchango huo wa fedha umechangia sana katika kutekeleza malengo ya Millenia kwa kupunguza vifo vya watoto kwa asilimia 4 kwa mwaka 2013 kwa kuboresha utoaji wa chanjo kwa watoto na tiba sahihi ya ugonjwa wa Malaria kwa kiasi kikubwa”. Alisema Dkt. Mmbando. Pia Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Jumanne Sagini amesema kuwa ameishukuru Serikali ya Uswisi kwa msaada walioupata na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumiwa katika kuboresha zaidi huduma ya Afya katika Mikoa iliyoongezwa kuanzia ngazi za Wilaya.

Mfuko wa pamoja wa Afya ulianzishwa nchini kwa lengo la kusaidia kuboresha huduma za Afya kwa kushirikiana na Serikali ya Uswisi pamoja na nchi zingine zilizoendelea ikiwemo Canada, Denmaki na washirika wengine wa maendeleo.

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.