2015-12-03 07:41:00

Papa atafakari ziara yake ya kitume Barani Afrika asema ; Afrika ni Kuzuri


Baba Mtakatifu  Francisko katika  Katekesi yake kwa Mahujaji na wageni Jumatano, alitoa muhtasari wa ziara yake ya Kitume ya hivi karibuni barani  Afrika. Hii ilikuwa ni ziara yake ya kwanza Barani  Afrika, na pia kufika barani Afrika, ziara aliyoianza tarehe 25 -30 Novemba 2015, kutembelea  nchi Tatu Kenya , Uganda na Jamhuri ya Afrika Kati.  Na amemshukuru Mungu kwa  zawadi yake kuu, iliyomruhusu kukamilisha ziara hiyo kwa amani na utulivu , na pia ametoa shukurani zake za dhati kwa wote waliofanikisha ziara hiyo  kwa namna moja au nyingine, kwa mamlaka za kiserikali , kwa Maaskofu, na wananchi kwa ujumla, akionyesha kutambua kwamba kulikuwa na kazi nyingi za ziada.

Baada ya shukurani za jumla , aliendelea kutazama nchi moja moja  akianzia na Kenya ,  akiitaja kwamba , ni  nchi inayowakilisha vizuri changamoto  za kimataifa kwa wakati wetu, hasa katika : kulinda viumbe na kuleta mageuzi  katika maendeleo kwa kuzingatia usawa na umoja  endelevu.  Maelezo ya Papa Francisco yalilenga katika kile alichokiona katika mji wa Nairobi, ambako kuna vyote viwili  Matajiri sana na Maskini sana wakiishi pamoja .  Ametaja hilo kwamba ni kashfa!  Na si barani  Afrika, lakini pia sehemu zingine duniani.  Papa amelaani moyo wa kupenda kushikamana na mali bila ya kujali maskini walio kandokando . Ameutaja  umaskini  kuwa ni  kashfa, na uwepo wake ni aibu kwa binadamu matajiri.

Na alieleza uzoefu wake alioupata wakati alipokutana na mamlaka na wanadiplomasia, ikiwa ni pamoja na wenyeji wa mtaani ;  viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo na dini nyingine, Mapadre ,  na Watawa, na vijana  wengi!  Katika kila tukio Papa amesema, alitiwa moyo na utajiri wa hazina ya  nchi hiyo katika yote mawili ,  utajiri wa asili na utajiri wa kiroho, na utajiri wa maadili kwa kizazi cha vijana ,ikionyesha hekima ya mfumo wa maisha ya watu wa Kenya . Na kwamba, kwa upande wake kwa  furaha aliwapatia neno la matumaini la Yesu Mfufuka, kwamba wasikatishwe tamaa na changamoto za  maisha lakini waweke matumaini na nguvu  zao katika imani,  wasikubali kuishi kwa  hofu, bali k atika tumaini, kama ilivyokuwa  kauli mbiu ya ziara  yake. Alihimiza kila siku kuishi kwa  unyenyekevu, toba na kusamehe kama maisha ya kawaida , na  kuheshimu wote hata wenye mamlaka. Na pia aliwataka watiwe moyo na ushujaa wa kuifuta imani yao kama ilivyokuwa kwa wahanga wa Chuo Kikuu  Garissa, waliouawa Aprili 2,  kwa sababu ya Ukristo wao. Papa ameomba damu yao  iliyomwangika, na iwe mbegu ya amani na udugu kwa Kenya, kwa Afrika na kwa dunia nzima.

 Baada ya maelezo hayo, Papa aliendelea na kituo cha Pili katika ziara hiyo, ikiwa ni  nchini Uganda, alikotembelea chini ya ishara ya Mashahidi wa Uganda waliotangazwa kuwa  Watakatifu miaka 50 iliyopita,  na  Papa Paulo VI.  Kwa sababu hiyo kauli mbiu katika tukio hili ilikuwa, “Mtakuwa mashahidi wangu" (Matendo 1.8).  Akiwa huko Uganda, Papa alihimiza waamini kupokea nguvu za Roho Mtakatifu, kwa sababu ni roho  anayeihamasisha mioyo, katika utendaji wa kazi za kitume.  Amesema,  siku alizokaa Uganda, aliziishi katika jotojoto  la ushuhuda, uliohasishwa na Roho Mtakatifu. Ushahidi kwa maana ya uwazi katika  utumishi wa Makatekista.  Papa ameshukuru dhamira yao iliyohamasishwa na Roho Mtakatifu na pia kwa familia zao  kwa ushuhuda huu wa upendo mkuu kwa Injili ya Kristo, unaofanywa na  jumuiya  na vyama na mshirika ya kitume mbalimbali katika huduma  kwa ajili ya maskini, walemavu na wagonjwa. Ushuhuda unaotolewa na vijana ambao, licha ya matatizo, wanaendelea  kuhifadhi zawadi ya matumaini na kujaribu kuiishi injili na si kwa mujibu wa dunia,  lakini kwenda kinyume na mambo ya kidunia na Kisasa.  Papa alieleza na kutaja makundi mbalimbali ya  Mashahidi  wa dini , wakiwemo Mapadre na watawa, wake kwa waume , ambao hutoa jibu lao la ndiyo kwa Kristo na kujitolea wenyewe kwa furaha katika  huduma  kwa  watu wa Mungu. Na kwa kundi jingine la Mashahidi alilosema, atatoa yake baadaye ,lakini kwao wote amesema, utendaji wao  huhamasishwa na Roho Mtakatifu katika kutoa huduma kwenye mahitaji mbalimbalii kama ilivyokuwa katika kazi za kupambana dhidi ya UKIMWI na katika mapokezi ya wakimbizi.

 

Mguu wa tatu wa safari yake ilikuwa katika Jamhuri ya  Afrika ya Kati, ambayo kijiografia ni moyo wa bara la Afrika, ambako alikwenda kwa nia ya kutoa ujumbe wa amani na mshikamano, unaoweza kuwatoa watu wa taifa hilo katika kipindi  kigumu sana cha mgogoro mkali na mateso kwa watu wa taifa hilo.. Kwa ajili hiyo, alipenda kuufungua Mlango wa Kanisa Kuu la Bangui  kama ishara ya imani na matumaini, wiki moja mapema, kabla  Kufungua Mlango  Mtakatifu wa Jubilee wa Huruma ya Mungu.  Papa ameeleza pia kwamba, apenda kuitumia nchi hiyo kama  kituo kikuu kwa ajili ya kutoa ujumbe wa imani na matumaini   na  kama mfano kwa wakazi wote wa Afrika,  wanaohitaji zaidi m zawadi ya ukombozi na faraja.  Ziara katika taifa hili aliifanya chini ya  Kauli Mbiu "Hebu twende ng’ambo ya pili " (Luka 8:22),  Maneno ya Yesu kwa wanafunzi wake .. "Nenda upande wa pili", kwa maana ya kiraia, ina maana kuacha nyuma  vita, mgawanyiko, umaskini, na kuchagua amani, maridhiano na maendeleo.  Huo ndiyo ulikuwa mchango wake katika maamuzi ya  jumuiya za kidini katika taifa hilo la Jamhuri ya Afrika Kati, ambako alikutana na  viongozi na wawakilishi mbalimbali wa  Kanisa la Kiinjili na Jumuiya na Muslim, na kushiriki pamoja katika sala na maombi na ahadi ya amani.  Na katika mkutano wake na Mapadre na watawa na vijana aliwaambia ni furaha iliyoje  kusikia kwamba , Bwana aliyefufuka yupo pamoja nao katika mashua, na ni yeye mwenye kuendesha gari hadi upande mwingine. Na amemshukuru Mungu aliyemwezesha kukamilisha ziara yake  katika uwanja wa Bangui, wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Mtume Andrew,  ambamo alitoa wito wa kufanya upya  ahadi ya  kumfuata Yesu, tumaini letu, amani yetu mbele ya  uso wa Huruma ya Mungu. 








All the contents on this site are copyrighted ©.