2015-12-03 08:00:00

Mwilisheni huruma na upendo kwa wagonjwa wa Ukimwi!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu Barani Afrika iwe ni fursa ya kumwilisha upendo na huruma katika huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi, ili wajisikie kwamba wanapendwa na kuthaminiwa, badala ya kuwanyanyapalia, hali inayowafanya kujisikia wapweke. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Desemba.

Inawezekana kutokuwa na maambukizi mapya ya Ukimwi Barani Afrika; kwa kupunguza vifo vya wagonjwa wa Ukimwi kwa njia ya kuwajali na kuwathamini. SECAM inakaza kusema, ubaguzi na unyanyapaa ni hatari sana kwa waathirika wa Virusi vya Ukimwi, kwani ni mambo yanayowafanya kujisikia kutengwa na jamii, kiasi kwamba, familia zinaficha ukweli kuhusu Ukimwi na vifo vya wagonjwa wa Ukimwi kwa kuogopa kutengwa na jamii. Ukweli na uwazi ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya Ukimwi.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia walikazia umuhimu wa utume wa familia hususan kwa familia ambazo zimetikiswa na ugonjwa wa Ukimwi, ili ziweze kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Kanisa. Ukimwi ni changamoto kubwa katika kukuza na kudumisha mafungamano ya kijamii Barani Afrika. Wanafamilia wanahamasishwa na Mama Kanisa kuonesha upendo na huruma kwa ndugu na jamaa zao walioathirika kwa Virusi vya Ukimwi. Iwe ni nafasi hata kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, linawajali na kuwahudumia waathirika wa Ukimwi.

SECAM inakumbusha kwamba, Kanisa Barani Afrika linaendelea kuadhimisha Mwaka wa upatanisho kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto ya haki, amani na upatanisho Barani Afrika iliyotolewa na Papa mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume, Dhamana ya Kanisa, “Africae munus”. Katika maandalizi ya uzinduzi rasmi wa Mwaka mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, SECAM inawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushuhudia imani yao kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya waathirika wa Virusi vya Ukimwi.

Familia ya Mungu Barani Afrika iendelee kushikamana kwa dhati katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi. Takimwi zinaonesha kwamba, nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara zimeathirika zaidi kwa ugonjwa wa Ukimwi. Inakadiriwa na Shirika la Afya Duniani kwamba, asilimia 70% ya maambukizi mapya ya Ukimwi duniani yako katika eneo hili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.