2015-12-03 11:29:00

Imani na matumaini ya maskini yalimlinda Baba Mtakatifu Francisko!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ni kati ya viongozi waandamizi waliokuwa wamefuatana na Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 25- 30 Novemba 2015. Hivi karibuni akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu amewagusia uzoefu wake kuhusu hija hii ya Baba Mtakatifu iliyokuwa inazingirwa na utata mkubwa wa ulinzi na usalama. Anasema, kulikuwepo na wadau mbali mbali waliohusishwa katika ulinzi na usalama, lakini imani, matumaini, ari na furaha ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, vilikuwa ni msaada na ulinzi tosha kabisa kwa Baba Mtakatifu Francisko kiasi cha kujisikia yuko nyumbani kati ya ndugu zake.

Kardinali Filoni anakaza kusema, kabla ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa M’poko, Bangui, waliweza kushuhudia magofu ya nyumba zilizoungua kwa moto au kutekelezwa kwa mabomu. Waliona wakimbizi na wahamiaji wakikimbilia kwenye Uwanja wa ndege kwani uwanja huu kwa sasa unazungumzwa na wakimbizi wanaohofia usalama wa maisha yao! Vikosi vya kulinda amani vilikuwepo ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na usalama barabarani. Wengi walisema kwamba, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilikuwa si mahali pa kwenda kwani hakuna uuhakika wa usalama.

Lakini Baba Mtakatifu Francisko alionesha utashi wake wa kibaba unaofumbatwa katika imani thabiti wa kutaka kwenda huko ambako hakuna ulinzi na usalama, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu alilindwa na watu waliokuwa daima wanazunguka gari na mahali pale alipokwenda kukutana na Watu wa Mungu kiasi cha kuwashangaza wengi, na kuwaacha wakiwa wamepigwa na bumbuwazi! Matendo makuu ya Mungu.

Ni watu hawa walioonja wema, huruma na ukarimu wa Baba Mtakatifu waliomsindikiza kwa sala na uwepo wao wa daima, kiasi hata cha kuhitimisha hija yake ya kitume Barani Afrika salama salimini! Kwa hakika watu walisali na kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake Barani Afrika! Uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, katika kipindi hiki ambacho hakuna uhakika wa ulinzi na usalama; wakati vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inaendelea kujionesha kutokana na udini, ukabila pamoja na uchu wa mali na madaraka, hapo ndipo Baba Mtakatifu alipoona panafaa kwa ajili ya uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Lengo ni kuwawezesha waamini kuvuka kwenda upande wa pili wa ng’ambo ya maisha, tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha unaojikita katika toba, wongofu wa ndani, msamaha, upatanisho, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni mwaliko wa kushuhudia imani katika matendo ya kila siku kwamba, kweli wamekuwa ni watu wapya. Katika mazingira kama haya alisema Baba Mtakatifu Bangui umekuwa kweli ni mji was ala na huruma ya Mungu kimataifa walau kwa siku moja! Kwani hapa walimwengu walikaza macho yao ili kuona kile kilichokuwa kinatendeka! Wengi wanasema, uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Bangui, ni tukio ambalo limeacha alama ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anakaza kusema daima maskini ndio walengwa wa Habari Njema ya Wokovu, hawa kwa njia ya maisha, sala na sadaka yao wanalitegemeza Kanisa katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu alipokuwa anahitimisha hija yake ya kitume Barani Afrika amewataka waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kumsindikiza katika maisha na utume wake katika sala na sadaka zao ili aweze kuwa Askofu wema na mtakatifu kadiri ya mfano wa Kristo mchungaji mwema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.