2015-12-02 08:33:00

Mheshimiwa Padre Vincenti Kirabo ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Hoima


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Vincenti Kirabo, Jaalimu kutoka Seminari kuu ya Ggaba, Kampala kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Hoima, nchini Uganda. Askofu mteule alizaliwa tarehe 1 Oktoba 1955 Jimboni Hoima. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre hapo tarehe 9 Septemba 1979 Jimboni Hoima. Tangu wakati huo amekuwa mwalimu na mkurugenzi wa miito Jimboni Hoima.

Kunako mwaka 1988 hadi mwaka 1990 alipelekwa na Jimbo nchini Marekani kwa ajili ya kujiendeleza zaidi katika masuala ya elimu na kufanikiwa kupata shahada ya uzamili katika elimu. Aliporejea nchini Uganda akapangiwa kuwa ni Paroko Msaidizi baadaye akateuliwa kuwa Gombera wa Seminari ndogo ya Mtakatifu Yohane Bosco, Jimbo Katoliki Hoima, utume alioutekeleza kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1992. Baadaye aliteuliwa kuwa mratibu wa fedha na uchumi, Jimbo Katoliki la Hoima na kunako mwaka 1998 hadi mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Buseesa.

Kunako mwaka 2003 hadi mwaka 2007 alipelekwa nchini Italia kwa masomo ya juu zaidi katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma na kujipatia shahada uzamili katika fani ya Taalimungu Maandiko Matakatifu. Aporejea nchini Uganda kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Katulikire. Mwaka 2008 hadi mwaka 2012 Alikuwa ni jaalimu na mchumi wa Seminari kuu la Alololum, Gulu, Uganda. Kunako mwaka 2012 hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu, amekuwa ni Jaalumu wa Maandiko Matakatifu Seminari kuu ya Ggaba, Uganda. Tangu tarehe 8 februari 2014 Jimbo Katoliki la Hoima limekuwa wazi kufuatia kifo cha Askofu Deogratias Byabazaire.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.