2015-12-02 15:39:00

Mapambano dhidi ya UKIMWI nchini Tanzania


Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani nchini Tanzania kwa mwaka 2015 imekuwa ni fursa kwa wanachi kupima afya zao. Katika tamko kwa maadhimisho haya, wadau mbali mbali wameonesha mafanikio yaliyokwisha kupatikana nchini Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi; wameonesha changamoto, matazamio na wito kwa Serikali ya Tanzania ili wagonjwa wote wenye virusi vya Ukimwi wapewe dawa za kurefusha maisha.

1.0: Utangulizi

Tarehe 1 Desemba ya kila mwaka, Dunia huwa inaadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani. Siku hii ni mahsusi kwa kuwakumbusha watu kwamba UKIMWI bado upo hivyo jamii haina budi kuendeleza mapambano dhidi ya janga hili. Siku hii pia imetengwa kwa ajili ya kuwakumbuka ndugu, jamaa na marafiki zetu waliopoteza maisha kutokana na vifo vinavyotokana na UKIMWI. Kaulimbiu ya ya mwaka huu ni ‘Tanzania Bila Maambukizi Mapya ya VVU, Unyanyapaa na Vifo Vinavyotokana na UKIMWI Inawezekana’. Tangu kuanza kwa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini zaidi ya miongo mitatu iliyopita, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi imepata mafanikio na na kukabiliana na changamoto mbalimbali katika mapambano hayo.

2.0: Mafanikio ya Nchi katika Mapambano dhidi ya UKIMWI

i. Kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya VVU kitaifa kutoka asilimia 7 mwaka 2003-2004 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2011-2012.

ii. Kwa mwaka 2014, jumla ya wajawazito 75,334 ambao ni sawa na asilimia 90 walipata dawa za kupunguza makala ya VVU yaani ARV kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU sambamba na kuboresha afya zao. Mafanikio hayo yanatokana na kutekeleza Mpango wa Option B+ ambao unatekelezwa katika vituo 5,361 sawa na asilimia 91 ya vituo vyote 5, 863 nchi nzima vinavyotoa huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto. Hii imepunguza maambukizi ya VVU kwa watoto wanaozaliwa na kina mama wenye maambukizi ya VVU kutoka asilimia 26 mwaka 2010 hadi asilimia 8.6 mwaka 2014, ambapo inaendana na lengo la kufikia asilimia chini ya 4 mwaka 2015.

iii. Hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu (2015), jumla ya wanaume 1,758,930 ambao ni sawa na asilimia 83.7 ya lengo la kufikia 2,102,252 mwaka 2015 walikuwa wametahiriwa katika mikoa 13 yenye viwango vya juu vya maambukizi ya VVU lakini yenye viwango vya chini vya tohara. Mikoa hiyo ni pamoja na Geita, Iringa, Kagera, Katavi, Mara, Mbeya, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu na Tabora.

iv. Jumla ya watanzania 27,267,920 walikuwa wamepata huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu (2015).

v. Inakadiriwa kuwa jumla ya watanzania 1,500,000 wanaoishi na VVU huku miongoni mwao watu 703,584sawa na asiliamia 47 walikuwa wanaendelea kutumia dawa za ARV wakiwemo watoto 46,035walio chini ya miaka 14 hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu (2015).

3.0: Changamoto

i. Kuendelea kwa maambukizi ya VVU kwa watoto wanaonyonyeshwa na kina mama wenye maambukizi ya VVU ambao hawana ufuasi mzuri wa Matumizi ya ARV.

ii. Kasi ndogo ya watoto wenye VVU waliosajiliwa kwenye vituo vya huduma za tiba na matunzo.

iii. Kasi ndogo ya wanaume watu wazima kujitokeza kupata huduma ya tohara kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU.

iv. Idadi ndogo ya wenza kujitokeza kupima Virusi vya UKIMWI kwa pamoja.

4.0: Matazamio

i. Kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa watoto kutoka asilimia 26 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 4 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu (2015). Juhudi zaidi zitawekezwa katika kuhamasisha ufuasi wa matumizi ya ARV kwa kina mama wajawazito na wanaonyonyesha.

ii. Kuongeza idadi ya watoto 27,500 walio kwenye tiba ya UKIMWI kwa kipindi cha miaka 2, kuanzia Oktoba 2014 hadi Septemba, 2016.

iii. Kufikia Idadi ya wanaume 2,102,252 watakaokuwa wametahiriwa ifikapo mwaka 2017 katika mikoa 13 yenye viwango vya juu vya maambukizi ya VVU sambamba na viwango vya chini vya tohara ya wanaume.

iv. Kuendelea kupanua huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU ikiwemo kuhamasisha wenza ili wale watakaobainika wana maambukizi waweze kupatiwa huduma za matunzo na tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

v. Kupanua wigo wa upatikanaji wa mashine za kupima wingi wa VVU mwilini (HIV Viral Load) sambamba na kupima chembe hai za damu aina ya CD4. Hii itapelekea kufikia lengo la kupima asilimia 50 ya watu wote walio kwenye tiba ifikapo mwaka 2017.

5.0: Wito: Wananchi wote, wakubwa kwa watoto, waendelee kujitokeza ili kupata huduma za Virusi vya UKIMWI na UKIMWI ambazo zinatolewa bila malipo nchini kote. Aidha, mashirika ya dini, asasi za kiraia, wadau mbalimbali kushiriki katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.