2015-12-02 11:55:00

Kasi ya kushughulikia rushwa na ufisadi Tanzania inatisha!!


Waziri mkuu wa Tanzania Kass M. Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambaye anamaliza muda wake, Bw. Juma-Alfani Mpango. Akizungumza na Balozi Mpango Jumatano, Desemba 2, 2015, ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alimshukuru Balozi huyo kwa pongezi zake na kumwomba aendelee kuwa balozi mzuri wa kuitangaza Tanzania hata baada ya kurejea nyumbani. Pia alitumia fursa hiyo kuwaombea heri na amani wananchi wa DRC pamoja na Rais Joseph Kabila katika maandalizi ya uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika nchini humo hapo mwakani.

Kwa upande wake, Balozi Mpango ambaye alisema amekaa nchini Tanzania kwa miaka 12, alimweleza Waziri Mkuu kwamba amejifunza mengi sana kutoka kwa viongozi wa Tanzania kubwa vikiwa ni uchapakazi na unyenyekevu. “Nimeona utawala wa Rais Benjamin Mkapa, Rais Jakaya Kikwete na sasa Dkt. John Pombe Magufuli. Ninavutiwa na hatua mnazochukua hivi sasa katika kupambana na rushwa na ufisadi,” alisema.

“Mambo niliyojifunza tangu nimekaa hapa ni uchapakazi na unyenyekevu. Unaona kabisa kwamba mtu anaamini kuwa madaraka siyo kitu cha kujivunia kwa mtumishi wa umma. Anachotakiwa kuwa nacho ni utayari wa kuwatumikia wananchi,” alisema kwa Kiswahili sanifu. Balozi Mpango aliomba mahusiano ya nchi hizi mbili yaendelezwe kwani DRC imekuwa ikinufaika na matumizi ya bandari ya Dar es Salaam katika kusafirishia bidhaa zake kwenda nchi za nje.“Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwetu. Mwaka 2004 tulisafirisha tani za mizigo 200,000, mwaka 2014 ziliongezeka na kufikia tani milioni 1.3; na mwakani tunataraji zitaongezeka na kufikia tani milioni tatu,” alisema.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,








All the contents on this site are copyrighted ©.