2015-12-01 09:50:00

Salam, matashi mema na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 30 Novemba 2015 amehitimisha hija yake ya kitume Barani Afrika ambako alipata bahati ya kutembelea Kenya, Uganda na Jamhuri ya watu wa Afrika ta Kati. Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu amepitia kwenye anga la Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Niger, Algeria, Tunisia na Italia. Baba Mtakatifu akipita katika maeneo haya amewatumia wakuu wa nchi salam, matashi mema na baraka zake za kitume!

Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru kwa namna ya pekee Rais wa Serikali ya mpito Catherine Samba-Panza wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kwa ukarimu mkubwa waliomwesha wakti alipokuwa nchini mwao. Anawahidia kuendelea kuwa karibu nao kwa njia ya sala na kwamba, anapenda kuwapatia baraka zake za kitume!

Baba Mtakatifu alipoingia kwenye anga la Chad, amewatakia heri na baraka wananchi wote wa Chad na kwamba, anawasindikiza katika hija yao ya maisha kwa njia ya sala na kwamba, anawapatia baraka zake za kitume! Haya amemwandikia Rais Idriss Dèby wa Chad. Akiwa njiani kuelekea Roma, Baba Mtakatifu Francisko alipowasili kwenye anga la Niger ametuma salam na matashi mema kwa wananchi wa Niger kupitia kwa Rais Mahamodou Issofou. Amewatakia heri, baraka na ustawi katika maisha yao .

Baba Mtakatifu alipoingia kwenye anga la Algeria amewakumbuka na kuwaombea wananchi wa Algeri pamoja na kuwatumia salam, baraka na matashi mema kupitia kwa Rais Abdelaziz Bouteflika. Anawaombea pia amani, ustawi na maendeleo. Baba Mtakatifu Francisko alipoingia Tunisia ametuma salam, matashi mema na baraka kwa wananchi wa Tunisia, akiwaombea baraka, amani na neema.

Baba Mtakatifu alipoanza kuiona anga ya Italia, amemwandikia ujumbe wa salam na matashi mema Rais Sergio Mattarella wa Italia, akimwelezea kuhusu hija yake ya kitume Barani Afrika ambako amepata nafasi ya kukutana na Familia ya Mungu Barani Afrika iliyokita mizizi yake katika Mapokeo ya maisha ya kiroho; wenye ari na moyo mkuu wa kutafuta maendeleo ya kweli. Baba Mtakatifu anamtakia Rais Mattarella na wananchi wote wa Italia utulivu na kwamba anawahakikishia sala na sadaka yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.