2015-12-01 10:19:00

Papa aweka jiwe la msingi la majadiliano, haki na amani Afrika ya Kati!


Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati imekuwa ni changamoto hata kwa viongozi wa Serikali na wanasiasa kwa ujumla wanaowania nafasi ya urasi nchini humo kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa amani na utulivu, kwa kujenga madaraja ya watu kukutana, tayari kusimamia ustawi na maendeleo yao kwa kuanza maisha mapya dhidi ya vita, chuki na mipasuko ya kisiasa.

Haya yamo kwenye barua ambayo imeandikwa na viongozi wa Serikali na wanasiasa nchini humo na kumkabidhi Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anahitimisha hija yake ya kitume Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Jumatatu, tarehe 30 Novemba 2015. Kuna wagombea 35 katika kiti cha Urais wakati wa uchaguzi na viongozi wengine watatu wanaotaka kuona uchaguzi unafanyika katika amani na utulivu.

Viongozi hawa walikutanika siku moja kabla ya Baba Mtakatifu kuwasili nchini mwao na hivyo kufanya maamuzi machungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wao. Wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa ujasiri wake wa kutekeleza ratiba yote iliyopangwa kwa ajili ya ziara yake nchini mwao, licha ya wasi wasi na mashaka kuhusu ulinzi na usalama. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko imekuwa ni msingi wa mchakato wa majadiliano unaojikita katika haki, amani na upatanisho.

Viongozi hawa wanapenda kumhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, watajitahidi kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu ili kufanikisha mchakato mzima wa uchaguzi mkuu kadiri ya Katiba na sheria za nchi, ili amani na utulivu viweze kutawala tena Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati! Juhudi hizi zimefanikishwa kwa msaada wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma. Jumuiya hii imekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhu ya amani katika migogoro ya kivita pamoja na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.