2015-11-30 13:21:00

Ujumbe wa Papa kwa Patriaki Bartholomeo wa I kwa Sikukuu ya Mtakatifu Andrea Mtume


Katika mwendelezo wa utamaduni wa kubadilishana  wajumbe katika maadhimisho ya Sikukuu ya Watakatifu Petro na Paulo, ambao ni wasimamizi wa Jiji la Roma, kila mwaka June 29 , na Sikukuu ya Mtakatifu Andrea Mtume msimamizi wa Jiji la Instanbul Uturuki, tarehe 30 Novemba, Baba Mtakatifu Francisko, ametoa salaam na ujumbe wake kwa Kanisa la Kiekumeni la Kiotodosi kupitia kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo,Patriaki Bartholomew I, katika kuiadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Andrea Mtume.

Kwa ajili ya tukio la sikukuu hii, Papa amewakilishwa na Kardinali Kurt Koch Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya uhamasishaji wa umoja wa Wakristo , na Katibu wa Baraza hilo Askofu mkuu Brian Farrel na Katibu mwandamizi Mons. Andrea Palmieri.

Salaam za Papa Francisko, ziliwasilishwa kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Kardinali Kurt Koch wakati wa kukamilika kwa maadhimisho ya Ibada ya Kiliturujia,  kwa ajili ya Sikukuu hii ya Mtakatifu Andrea Mtume,  ujumbe uliotiwa saini na yeye mwenyewe Papa, ambamo kwanza amemshukuru Mungu kwa kupita kipindi cha mwaka mzima tangu walipofanya adhimisho hili wakiwa pamoja katika Kanisa Kuu la Kipatriaki la Phanar la Istanbul Uturuki. Tukio aliloiita kuwa  wakati wa neema  ulio waruhusu kufanya upya na kuimarisha imani yao, kupitia  sala na maombi ya pamoja na kukutana kwao ana kwa ana, na kujenga mshikamano na umoja zaidi wa kirafiki kati yao na Kanisa wanalo liongoza kama mwalimu wakuu. Papa amekiri kwamba, tukio hili ni  uzoefu hai wa Kanisa usiokoma kushuhudia manufaa ya  imani kwa Yesu Kristo, Bwana mmoja, Mkombozi wa wote.

 Papa ameomba radhi kwa yeye mwenyewe kutoshiriki katika maadhmisho ya Sikukuu hii aliyotaja kuwa muhimu na hivyo akaomba ujumbe alioutuma upokewe kama ishara ya kuonekana ya upendo wake wa  kidugu na ukaribu wa kiroho wa Kanisa la Roma kwa  Patriaki na kwa wajumbe wote wa Sinodi Takatifu ya Kiotodosi na  viongozi wa dini, watawa na waamini wote wa Upatriaki wa Kiekumene wa Kiotodosi.

Baba Mtakatifu Francisco ameendelea kuutaja usharika wa kina katika imani na  upendo, akishukuru kwa yote yaliyokamilishwa kwa kudra ya Mungu,kwa ajili yao,  akiikumbuka pia  kupita kwa miaka hamsini ya azimio la Pamoja la Kanisa Katoliki-Kanisa la Kiorthodosi lililofanikishwa kwa pamoja  na viongozi wa Makanisa haya mawili , Papa Paulo VI na Patriaki wa Kiekumene  Athenagoras, akitaja pia kumbukumbu za kihistoria  zililzoleta utengano katika Kanisa mwaka 1054. Kashfa msingi, zilizo ongozana matukio ya kusikitisha katika kipindi hicho na kuendelea kuwa kikwazo kwa karne nyingi, katika kurudisha mahusiano chanya na upendo wa kidugu kati ya Wakatoliki na Waotodosi. 

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake ameomba  mapenzi ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye aliomba kwa Baba katika usiku wa mateso yake,  Wanafunzi wake  wawe na umoja" (Yn 17:21). Amesema ndivyo ilivyokuwa kwa Papa Paulo VI na Patriaki  Athenagoras , walitupilia mbalimbali kumbukumbu hizi za maumivu, na kusahau mantiki ya uhasama, kutoaminiana, uadui , chuki na kutengana badala yake wakajenga mantiki ya upendo na umoja, mshikamano na kukumbatiana kidugu.

Papa ameeleza na kurudia kutoa mwaliko kwa waamini wote wa makanisa haya mawili, kujiunga katika safari moja ya kuelekea katika  kurudisha upya ushirika kamili katika maisha ya Kanisa moja Takatifu Mwili wa Kristo katika imani, udugu na maisha ya kisakramenti miongoni mwao waamini. kama ilivyokuwa katika Kanisa la mwanzo .  Na kwamba, baada ya kurejeshwa uhusiano wa upendo na udugu, katika roho ya kuaminiana, heshima na upendo, hakuna tena kikwazo chochote katika ushirika wa Kiekaristi, kupitia maombi, usafi moyo, mazungumzo na ukweli. Papa anasema kwa hakika, ambapo maisha ya kanisa yanakubatia upendo wa Kristo, chanzo na hatima yake  siku zote ni katika upendo  wa Kiekaristi..

Papa ameendelea kuhimiza katika ujumbe wake , kwa ajili ya maendeleo katika safari  ya kuelekea ushirika kamili, hamu ya wote kwamba, wanahitaji kuendelea kuteka msukumo huo, kutoka ishara ya maridhiano na amani iliyoonyeshwa na Watangulizi wao,  Papa Paulo VI na  Patriaki Athenagoras I, na kwa sasa iwe katika  ngazi zote na katika kila mazingira ya maisha ya Kanisa na  mahusiano kati ya Wakatoliki na Waodosi, ni lazima wazidi kutafakari mantiki ya upendo kwamba, haina nafasi na roho ya ubinafsi. Mazungumzo ya kiteolojia yenyewe ni lazima yawe  endelevu katika  upendo  na kuheshimiana, lazima kuendelea kuchunguza kwa makini hoja zinazoendeleza mgawanyiko,   daima kwa lengo la kukuza uelewa wa pamoja juu ya  ukweli uliofunuliwa. Motisha ya upendo wa Mungu, ni lazima iwe kushuhudia  uaminifuwa imani kwa pamoja kwa  dunia, katika  ufanisi wa shuhuda kwa  ujumbe wa Kristo wa kukomboa na  maridhiano.

Papa ameeleza na kusema kwamba, leo hii dunia ina haja kubwa ya maridhiano, hasa katika mwanga wa damu  ya mashahidi  inayoendelea kumwagika katika mashambulizi ya kigaidi hata katika nyakati zetu. Kwa ajili hiyo, Papa anasema, hili  linadai waamini kuongozana waathirika wote,  kupitia sala, maombi na huduma, na katika kufanya upya ahadi za kudumisha  amani ya kudumu,  kwa kukuza majadiliano kati ya madhehebu na staraabu za kidini, kwa kuwa "kutojali au kukosa ufahamu kunaweza ongoza tu katika kutoaminiana na hata uwepo wa migongano na mgogoro mbaya isiyokuwa na maana.

Kwenye ujumbe huu Papa hakuchelea kutoa shukrani zake za dhati kwa dhamira na bidii ya Patriaki Bartholomew katika kujali suala muhimu la huduma kwa ajili ya viumbe, bidii zinazoonekana katika ishara ya uwepo wa siku ya maombi ya pamoja ya  Wakatoliki na Waotodosi ambayo imeanzishwa katika uwepo wake wa kila mwaka tarehe Moja Septemba,ili binadamu aweze kujali na kuwajibika katika kutunza na kuhudumia viumbe na mazingira inavyopaswa kwa manufaa ya wote na ya kudumu kwa vizazi vyote. Katika suala hili, Papa amesema ataukumbuka katika sala zake, kuombea  mkutano muhimu ya kimataifa juu ya mazingira unaofanyika  Paris na kwa ajili ya wote wanaoshiriki katika mkutano huo.

Papa alikamilisha ujumbe wake kwa kutaja  umuhimu wa Utume wa Partriaki BartholomewI  akisema , utakatifu wa kazi yake, inakuwa ni  wajibu katika kumsaidia binadamu, kugundua upya siri ya huruma ya Mungu na katika kuwa  daraja linalomwunganisha Binadamu na Mungu, na katika kuufungua moyo  kwa matumaini ya kupendwa  milele na  Mungu, licha ya hali yetu ya dhambi" (Misericordiae Vultus, 2). Kwa sababu hiyo, Papa ametoa  wito kwa watu wote kwamba, Mwaka Mtakatifu wa Jubilee ya Huruma ya Mungu,tunaouanza hivi karibuni ,  ni wakati wa kufaa, kutafakari  msamaha wa Mungu , uliobainishwa kikamilifu kupitia Mwana wake, Yesu Kristo, na sisi wenyewe tunapaswa kuwa  ishara za upendo wa Mungu kupitia msamaha wetu kwa wengine  pamoja na matendo ya huruma.  Papa ametaja hilo pia  kuwa ni dira maadhimisho ya kumbukumbu ya  kihistoria ya  Azimio la pamoja la  Kanisa  Katoliki na Kanisa la Kiotodosi, kuhusu kuondolewa kwa vikwazo vilivyotenganisha Kanisa mwaka 1054. Amesema, ni lazima kutembea katika njia iliyoanzishwa na Papa Paulo VI na Patriaki Athenagoras. Wakatoliki na Waotodosi, leo hii ni lazima kuomba msamaha wa Mungu na pia kuombana msamaha mmoja kwa mwingine, na hivyo kuungana pamoja kama Wakristo, wakiuonyesha mwili mmoja wa Kristo.

Papa ameeleza na kuwaomba waamini wote wa Upatriaki wa Kiekumene,  kuomba  ili Jubilee ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, uweze kutoa  matunda ya mengi mazuri ya kiroho, kama yalivyo matamanio ya Kanisa.  Papa amewahakikishia sala zake kwa ajili ya matukio ya Kanisa katika mwaka ujao, ikiwemo Sinodi Kuu ya Kiotodosi.  Papa ameonyesha matumaini yake kwamba, pengine tukio hilo muhimu kwa makanisa yote Kiotodosi,  litaweza kuwa chanzo cha baraka tele kwa maisha ya Kanisa.

Na kwa upendo wa kidugu na umoja katika Bwana,  Papa Francisko amewahakikishia ukaribu wake wa kiroho katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtume Andrea, akiwatakia kila la heri , fanaka na amani katika Bwana Yesu Kristo.

Na TJM.








All the contents on this site are copyrighted ©.