2015-11-30 10:09:00

Sisi sote ni ndugu, tushikamane kujenga nchi ili iwe ni mfano wa kuigwa!


Baba Mtakatifu Francisko ameianza siku yake ya pili kwenye Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, tarehe 30 Novemba 2015 kwa kutembelea Msikiti mkuu wa Koudokou ili kukutana na kuzungumza na Jumuiya ya waamini wa dini ya Kiislam nchini humo. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha udugu na kwamba nchi hii inaweza kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine Barani Afrika katika mchakato wa ujenzi wa amani! Baba Mtakatifu Francisko ametumia muda huu kutoa shukrani zake za dhati kwa kukutana na Jumuiya ya Waislam inayoongozwa na Imam Tidian Moussa Naibi. Waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo wanapaswa kujisikia wamoja ili kujnenga na kudumisha udugu, umoja na mshikamano, tayari kuchakarika katika ujenzi wa nchi yao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, vita na machafuko yaliyojitokeza nchini humo kimsingi hayana chanzo chake katika masuala ya kidini kwani waamini wa dini hizi mbili kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi kwa amani na utulivu, huku wakiheshimiana na kusaidiana. Hii ni changamoto ya kuendelea kushikamana ili kuondokana na vitendo vinavyoharibu sura ya Mwenyezi Mungu; matendo yanayotumiwa na baadhi ya watu kwa ajili ya mafao yao binafsi. Umefika wakati kwa waamini wa dini mbali mbali kukataa vita, chuki na tabia ya kulipizana kisasi kwa misingi ya udini na badala yake wasimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani, kwani Mungu ni amani.

Baba Mtakatifu anawapongeza viongozi wa kidini nchini humo kwa mchango wao katika mchakato wa majadiliano yanayopania kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba mazungumzo ya wadau mbali mbali nchini humo yataweza kusaidia ujenzi wa umoja wa kitaifa. Anawahimiza waamini wote kujenga mazingira ambayo yatasaidia Afrika ya Kati kuwa ni mahali pa ukarimu pasi na ubaguzi wa kikabila, kidini na kiitikadi.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwatia moyo wananchi wa Afrika ya Kati kujenga matumaini na kwamba, wakitaka wanaweza kuondokana na machafuko yaliyoko nchini mwao. Jambo hili linawezekana ikiwa kama wananchi wote watashirkiana kwa hali na mali na hivyo kuwa kweli ni chachu ya matumaini kwa nchi nyingine Barani Afrika. Huu utakuwa ni msaada mkubwa katika kumaliza kinzani na migogoro ya kivita inayoendelea kusikika sehemu mbali mbali za Bara la Afrika, ili kutoa nafasi ya mchakato wa maendeleo kuanza kushika kasi kwa ajili ya ustawi wa wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.