2015-11-30 14:28:00

Njia kuu za ukwepaji wa kulipa kodi katika Bandari ya Dar zatajwa


Serikali mpya nchini Tanzania inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli, inaendelea na kasi yake katika kupambana na uhalifu mbalimbali uliokuwa umekithiri ikiwemo rushwa na ukwepaji wa kulipa kodi.

Habari zilizoandikwa katika mitandao ya habari zinaeleza kinachoendelea katika kashfa ya kupitisha makontena 349 kwenye Bandari ya Dar es Salaam bila ya kulipiwa kodi, kwamba, idadi hiyo ya makontena ni sehemu ndogo tu ya mamia ya mizigo inayovushwa kinyemela kila siku na hivyo kuikosesha serikali mabilioni ya fedha.

Kama hatua za kupambana na uozo huo,  taarifa zinasema, mwishoni mwa wiki, serikali ya  Rais Magufuli imechukua  hatua kadhaa za kukomesha ukwepaji kodi katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwemo baadhi ya viongozi wake kusimamishwa kazi akiwemo  Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), Rished Bade, ambaye amesimamishwa kazi na anashikiliwa polisi kuhusiana na taarifa za serikali kukosa mapato takriban Sh. bilioni 80 kutokana na makontena 349 yaliyopitishwa bila kulipiwa kodi. Kadhalika, vigogo wengine kadhaa wa TRA wamesimamishwa kazi,  pia na  baadhi wanashikiliwa na polisi, ili kuwezesha i uchunguzi zaidi kuhusiana na kashfa hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Nipashe, unataja uwepo wa  njia nyingi zinazotumiwa na watu hawa kufanikisha hujuma hizi kwa manufaa binafsi.  Kati ya njia hizo zimetajwa kuwa ni pamoja na utumiaji wa mfumo wa zamani wa malipo ambao siyo sawa  na mfumo wa kisasa wa elektroniki, maarufu kama ‘E-Payment’. Mfumo huo wa zamani , unapendwa kutumiwa na wafanyabiashara  wasioaminifu , kwa kuwa kuwa,  maelezo yake huandikwa kwa mkono na hivyo ni rahisi kuufinyaga  ukweli kwa manufaa ya kukwepa   kodi.

Njia ya pili ya kuhujumu mapato bandarini hapo, imetajwa kuwa ni ya kushirikiana na maafisa wa benki. Tatu, ni mwanya wa uvushaji wa makontena yenyewe yasiyolipiwa ushuru kupitia mageti maalum yanayofahamika kwa kazi hiyo.  Nne ya kuhujumu kodi ya mapato  kwa  kuwatumia watu wanaoendesha bandari kavu (ICD’s). Tano ni ubadilishaji wa taarifa wakati wa kukadiria kodi inayotakiwa kulipwa. Sita ni kuanzishwa kwa kampuni ndogondogo za  vigogo wa TRA, kuondoa  mizigo bandarini. Nane ni mzigo kutolewa taarifa za uongo kama mzigo unasafirshwa nje ya nchi kwa mfano Malawi, wakati ukweli ni mzigo huo hubaki Tanzania. Na tisa ni  ubabaishaji unaofanyika katika kuorodhesha idadi ya makontena yanayotolewa bandarini kwenda kwenye bandari kavu. Aidha imedaiwa uwepo wa uzembe katika kufuatilia taarifa za ukaguzi ambazo zimekuwa zikiishia kubaki kama makabrasha bila utekelezaji wowote kwa yaliyopendekzwa na watalaam.

Mwenyekiti wa Chama kinachowaunganisha Wafanya biashara Tanzania, Johnson Minja,  ametaja  ukwepaji wa kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara  hasa mashuhuri nchini Tanzania kimekuwa ni kilio chao cha muda mrefu na sasa wanafurahi kuona kuwa serikali mpya imelivalia junga suala hilo. Anatumaini hatua zinazochukuliwa hazitakuwa mvua za vuli zenye kunyesha na kukatika mara.

Taarifa nyingine inayofanana na hiyo inaeleza kuwa,  kama hatua ya kukomesha wizi wa dawa katika bohari kuu ya dawa ya serikali na kuuzwa katika maduka binafsi, kwa sasa vidoge vyote vinavyotoka katika Bohari hiyo, zinazo lengwa kutumiwa katika hospitali za serikali, kwa sasa kila kidoge kitakuwa na  nembo maalum ya serikali “GOT”.   Mkuu wa Kitengo hicho Bwanakunu, ametaja baadhi ya dawa zilizowekewa alama hiyo kuwa ni Diclofenac, Amoxillin, Ciprofloxacin, Contrimoxale, Paracetamol na Magnesium.








All the contents on this site are copyrighted ©.