2015-11-29 11:52:00

Salam na matashi mema kwa wananchi wa Uganda, DRC na Afrika ya Kati!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 29 Novemba 2015 akiwa njiani kuelekea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati amebahatika kuruka katika anga la Uganda, DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Wakati wote alipokuwa anapita katika nchi hizi amewatumia Marais wake salam, matashi mema na ustawi. Akiwa kwenye anga la Uganda, Baba Mtakatifu amemshukuru Rais Yoweri Kaguta Museveni pamoja na wananchi wote wa Uganda katika ujumla wao kwa ukarimu waliomwonesha wakati alipokuwa miongoni mwao. Anapoelekea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kuendelea na hija yake ya kitume anasema anapenda kuiombea Uganda amani, furaha na ustawi.

Baba Mtakatifu alipoingia kwenye anga la DRC amemtumia salam Rais Joseph Kabila pamoja na wananchi wote wa DRC. Amewaombea wananchi wote wa DRC baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwakirimia amani na ustawi. Baba Mtakatifu Francisko alipoingia kwenye anga la Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati amemtumia salam na matashi mema Rais wa mpito Catherine Samba-Panza. Baba Mtakatifu anatumaini kwamba, atafurahia sana uwepo wake kati yao na kwamba, anawatakia baraka wananchi wote wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.