2015-11-29 16:56:00

Papa asema: Dumisheni umoja wa kitaifa, onesheni ujasiri wa kuanza upya!


Baba Mtakatifu Francisko na ujumbe wake wamewasili nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati na kupokelewa na viongozi mbali mbali wa Serikali na Kanisa waliokuwa wanaongozwa na Mama Catherine Samba-Panza, Rais wa mpito nchini Afrika ya Kati. Baba Mtakatifu amepigiwa mizinga ishirini na moja, kisha akamtembelea Rais wa mpito Ikulu na hatimaye, kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanasiasa pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchini zao kwenye Jamhuri ya Afrika ya kati.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake ya kwanza nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja wa nyumba ya wote; wawe na ujasiri wa kuanza ukurasa mpya wa maisha kwa kujikita katika umoja, utu na kazi na kwamba, Kanisa litaendelea kutekeleza dhamana na utume wake nchini humo. Hotuba ya Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee imejikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa kitaifa, changamoto ambayo inawashirikisha mashirika ya kimataifa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, ili kukuza na kudumisha mshikamano na ushirikiano kati ya watu.

Umoja wa kitaifa ni muhimu sana ili juhudi hizi ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Umoja wa kitaifa uwakumbatie wananchi wote wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati katika tofauti zoa, ambazo ni utajiri mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Nchi hii inapaswa kuendeleza mchakato wa upatanisho; kuweka silaha chini ili kudumisha msingi wa amani; kuboresha huduma za afya na elimu kwa ajili ya wananchi wote sanjari na kuboresha misingi ya utawala bora katika hatua mbali mbali za uongozi wa nchi.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mchakato wa majadiliano ya umoja wa kitaifa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni uiwezeshe nchi kuanza ukurasa mpya wa historia yake kwa kukazia zaidi: umoja wa kitaifa; utu na heshima ya binadamu pamoja na kazi mambo msingi katika nembo ya Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Umoja wa kitaifa ujengeke katika msingi wa utofauti wao kwa kuondokana na woga usiokuwa na mashiko; ukabila ambao ni sumu ya mafungamano ya kijamii; itikadi za kisiasa zinazowagawa watu bila kusahau udini sumu ya amani na utulivu. Umoja katika utofauti ni changamoto endelevu katika maisha ya mwanadamu inayohitaji kipaji cha ugunduzi, ukarimu, unyenyekevu na heshima kwa wengine. Yote haya yanapaswa kufanyika ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu wa binadamu kwa kuwa na huduma bora za afya; kwa kupambana na utapiamlo wa kutisha; kwa kuwa na makazi bora ya watu. Huu ndio mkakati unaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ili kudumisha utu wa binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, nchi hii imebahatika kuwa na maliasili nyingi zinazoweza kutumika kutoa fursa za kazi ili kuboresha maisha ya kifamilia. Viongozi wanapaswa kuwajibika na kuwa makini katika matumizi ya rasilimali na maliasili Barani Afrika. Huu ni wajibu fungamanishi kwa wananchi wote, serikali na washirika katika mikakati na sera za maendeleo kwa Bara la Afrika. Kumekuwepo na uporaji mkubwa wa rasiliali ya Afrika, hali ambayo pia inachangia kuharibika kwa mazingira, nyumba ya wote. Ili kazi iweze kuchangia katika mchakato na ustawi wa wengi haina budi kusimikwa katika msingi wa mshikamano.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbee katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji ya mtu mzima:kiroho na kimwili. Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja wa kitaifa, utu wa binadamu na kazi. Baba Mtakatifu anapenda kuungana na Maaskofu kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ili kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika mchakato wa amani na upatanisho, ili kila mtu aweze kuendelea na kuendelezwa kama alivyowahi kusema Mwenyeheri Paulo VI, kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki wa kwanza kufika Barani Afrika ili kutia shime mwanzo wa kurasa mpya za maendeleo Barani Afrika. Baadaye, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea Kambi ya wakimbizi na kuzungumza na wakimbizi hawa. Baba Mtakatifu na msafara wake wameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa chakula cha mchana.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.