2015-11-29 17:43:00

Jengeni umoja unaojikita katika huduma na Uinjilishaji dhidi ya mipasuko!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Jumapili tarehe 29 Novemba 2015 amekutana na kuzungumza na Jumuiya za Kiinjili kwenye Kitivo cha Taalimungu ya Kiinjili, FATEB kilichoko Bangui. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee umoja unaojionesha katika huduma kwa Kristo Yesu; umuhimu wa Uinjilishaji na umoja kama jibu makini dhidi ya kinzani na migawanyiko.

Baba Mtakatifu amewatakia matashi mema wajumbe wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili Afrika ya Kati na kwamba, yuko kati yao kama ndugu. Amewakumbusha kuwa Wakristo wote wako kwa ajili ya kumhudumia Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu anayewaunganisha kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Wakristo wote wanachangamotishwa kujifunga kibwebwe tayari kutoka kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi ambao wanatembea katika giza la kinzani, vita na mateso mengi.

Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu hana ubaguzi kwa wale wote wanaoteseka na kusumbuka kwa matatizo mbali mbali. Jumuiya zote za waamini zinateseka kwa pamoja pasi na ubaguzi; zinateseka kwa kukosa haki; kutokana na chuki na uhasama unaopandikizwa na Shetani. Baba Mtakatifu ameonesha mshikamano wake kwa Mchungaji Nicolas ambaye hivi karibuni nyumba yake ilichomwa moto pamoja na kituo chake cha sala.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, umoja na mshikamano ni silaha madhubuti dhidi ya chuki na uhasama kati ya watu, changamoto kwa Wakristo kushikamana na kuanza kutembea katika njia ya umoja, jambo msingi hata katika maisha ya kiroho. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya neema ya umoja na kwamba, watoto wake wote wanateseka na wanahitaji kushikamana kwa ajili ya huduma makini kwa ndugu zao. Kwa uchungu Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, utengano miongoni mwa Wakristo ni kashfa dhidi ya utashi wa Kristo Yesu anayewataka wafuasi wake kuwa wamoja kama Yeye alivyo na umoja na Baba yake wa Mbinguni. Hii ni kashfa inayojionesha machoni pa vita, chuki na uhasama unaoendelea kusababisha mateso makali kwa binadamu; mambo ambayo kimsingi ni kinyume kabisa cha Injili ya Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.