2015-11-28 16:46:00

Huduma kwa maskini ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa!


Nyumba ya Upendo ya Nalukolongo ilianzishwa na Hayati Kardinali Emmanuel Kiwanuka Nsubuga wa Jimbo kuu la Kampala, Uganda na mwanzilishi wa Shirika la Watawa Msamaria mwema. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 28 Novemba 2015 amepata nafasi ya kutembelea katika nyumba hii na kusalimiana na watawa pamoja wagonjwa wanaohudumiwa na watawa hawa. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa huduma kwa maskini, wagonjwa na walemavu; akazitaka Parokia na Jumuiya mbali mbali nchini Uganda kutoa huduma kwa maskini.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa amewashukuru watawa wanaotoa huduma kwa maskini, wagonjwa na walemavu katika hali ya ukimya na furaha bila kuvisahau vyama vya kitume na watu wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa ndugu zao wahitaji hususan wagonjwa wa Ukimwi. Ikumbukwe kwamba, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu na maisha pamoja na utume wa Kanisa. Nyumba ya upendo ni mahali ambapo watu wanaonja huduma ya upendo wa Mungu na kwamba, yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, hukumu yake itajikita katika matendo ya huruma!

Baba Mtakatifu akiwa kwenye nyumba ya upendo, anawaalika waamini katika Parokia na Vyama vya kitume nchini Uganda na katika Kanisa Barani Afrika kuhakikisha kwamba wanawakumbatia na kuwahudumia maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lengo ni kupambana na ubinafsi, uchoyo na ubaguzi unaoendelea kuenea kwa kasi katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anazitaka familia za Kikristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa chachu ya upendo mnyenyekevu na huruma ya Mungu kwa waja wake, hasa kwa watoto, wazee na wote wanaohitaji msaada wao wa hali na mali. Parokia na Jumuiya za Kikristo, kamwe zisizibe masikio na kufunga mioyo yao kwa ajili ya kusikiliza kilio cha maskini! Huduma hii inaweza kutekelezwa katika maisha ya kawaida pasi na makuu kwa kutambua kwamba, hii ndiyo njia sahihi ya ufuasi wa Kristo. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kusaidia mchakato wa nguvu ya Kristo kuingia duniani ili kuleta mabadiliko ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.