2015-11-27 11:50:00

Nendeni mkasilikize kilio cha maskini wa Kangemi!


Baba Mtakatifu Francisko ameianza siku ya tatu ya hija yake ya kitume nchini Kenya kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Kenya na baadaye kwenda kutembelea na kuzungumza na wananchi wanaoishi katika kitongoji cha watu maskini cha Kangemi, nje kidogo ya Jiji la Nairobi. Akiwa Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Kangemi, Baba Mtakatifu ametia sahihi kwenye kitabu cha wageni, amesali na kuangalia cinema inayoonesha hali ya maisha ya wananchi wa Kangemi.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia nafasi hii kuwashukuru wenyeji wake kwa kumpokea na kumkaribisha kati yao na kwamba akiwa kati yao anajisikia kuwa ni ndugu yao na kwamba neno hili analisema kutoka katika sakafu ya moyo wake na wala haoni aibu kulitamka na kwamba, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wake na kwamba, Kanisa litaendelea kulaani vitendo vyote vinavyopelekea ukosefu wa haki msingi za kijamii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema anafahamu utamaduni wa watu wanaoishi katika vitongoji vya watu maskini; utamaduni unaojikita katika upendo na mshikamano wa dhati; usioangalia fedha bali utu na heshima ya binadamu; tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani. Ni maeneo ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo pamoja na kuhakikisha kwamba, marehemu hata katika umaskini wao wanazikwa kwa heshima zote. Hapa ni mahali ambapo wagonjwa wanapata tunza na huduma ya upendo; watu wanagawana na kushirikishana hata kile kidogo walicho nacho!

Baba Mtakatifu anafafanua zaidi kwamba, hekima ya utamaduni wa watu wanaoishi katika maeneo ya watu maskini ndani ya jamii inaambata tunu msingi za Kiinjili, tofauti kabisa na maisha ya mijini ambako ni patashika nguo kuchanika; sehemu ambazo zinajitambulisha kwa kuwa na ulaji wa kupindukia. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia watu wote wanaoishi katika makazi duni watambue kwamba wanapendwa na kuheshimiwa na Yesu na kamwe hawezi kuwasahau. Yesu alianza maisha na utume wake, pembezoni mwa mji kwa maskini kwa ajili ya maskini pamoja na maskini ili aweze kuwafikia watu wote!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, yote haya hayawezi kuhalalisha ukosefu wa haki na makazi duni yanayowakumba watu wengi katika maisha yao. Kuna watu wachache ndani ya jamii wenye nguvu ya kisiasa, kiuchumi na wanaendelea kutanua kana kwamba hakuna kifo, wakati ambako makazi duni yanaendelea kuongezeka na hivyo kuhataraisha maisha, afya na usalama wa wengi. Hapa kuna ugawaji na matumizi mabaya ya ardhi; kuna watu wanamiliki maeneo makubwa ya ardhi kwa mafao ya binafsi. Kwenye makazi duni bado kuna kosekana miundo mbinu na huduma msingi kwa wakazi. Haya ni mambo kama vile barabara na mitaa safi; zahanati na shule; maeneo ya michezo na burudani, lakini zaidi kuna ukosefu wa maji safi na salama. Hapa ni uwanja wa mapambano ambamo wanawake wajasiri wanaendelea kusimama kidete kuwalinda na kuwatunza watoto wao dhidi ya hatari zinazoweza kuwaandama katika maisha. Yote haya ni matokeo ya ukoloni mamboleo ambao unaendelea kuligawa Bara la Afrika ili kuwanufaisha watu wachache.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, hususan viongozi wa Kanisa kuamsha ari na moyo wa kimissionari ili kusimama  kidete kupinga ukosefu wa haki msingi za binadamu, kwa kuguswa na matatizo pamoja na mahangaiko ya maskini, tayari kujibu kilio chao kwa kuwasindikiza katika mapambano yao, kulinda na kuhifadhi matunda ya kazi zao za pamoja sanjari na kusherekea ufanisi unaopatikana. Baba Mtakatifu anatambua mchango mkubwa unaofanywa na viongozi wa Kanisa lakini anawakumbusha kwamba, maskini ndio walengwa wa Habari Njema ya Wokovu! Baba Mtakatifu amewapatia kiasi fulani cha fedha ili kuboresha huduma msingi katika kitongoji cha Kangemi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.