Umoja , mshikamano na amani kati ya Wakristo na Waislamu barani Afrika , siyo tu vinawezekana, lakini ni ukweli halisi, kwa kuwa hakuna dini yenye kuwa na uwezo wa kufuta dini nyingine. Ni maelezo yaliyotolewa hivi karibuni na Askofu Mkuu Ignasius Kaigama wa Jimbo Kuu la Jos Nigeria, ambaye pia ni Rais a Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria. Askofu Mkuu Ignasius Kaigama alieleza hilo, katika mhadhara wa Chuo Kikuu cha DePaulo cha Marekani hivi karibuni juu ya Mada "Waislamu na Wakatoliki katika Mazungumzo: Matarajio, Fursa na Changamoto. Mhadhara huo uliandaliwa na Kituo Katoliki cha Utamaduni na Theolojia katika Chuo Kikuu cha DePaulo.
Katika Maelezo yake aliisisitiza kwamba, "Ukristo na Uislamu lazima kutembea pamoja kwa kuwa waamini wa dini hizi mbili wote hutumia "Neno amani. Amani kama moja ya nguzo muhimu katika imani ya dini hizi. Daima huhimiza amani na kamwe vita. Kwa imani hiyo, mazungumzo kati ya makundi haya mawili , yanawezekana na hakuna sababu zinazoweza tosheleza kusema yasiwepo, iwapo wote wanazungumza lugha moja ya amani.
Maelezo ya Askofu Mkuu Kaigama, yalionyesha pamoja na uwepo wa migogoro mingi na vurugu, katika ukweli wake wa ndani hakuna sababu za kidini lakini ni vurugu na migongano inayolishwa na chuki za kisiasa au kikabila na masuala mengine yanayosababisha umaskini na uhaba wa rasilimali, ingawa inaweza pambwa na watu kama ni migongano ya kidini.
Askofu Mkuu Kaigama, alionya kila mmoja kushikilia imani yake, kama njia iliyo bora katika kuyaongoza maisha bila kuingilia imani ya wengine. Na alihitimisha kwa kutoa ombi kwa viongozi Wakristo na Waislamu 'kuhakikisha hakuna uhasama wala vurugu katika kukabiliana tofauti zinazoweza jitokeza, badala yake watumie njia ya majadiliano na kuheshimiana .
Na Ijumaa hii Novemba 27, majira ya jioni katika Chuo Kikuu Katoliki ya Moyo Mtakatifu cha Milan, katika ukumbi wa Pius XI, kutafanyika Mkutano kuzungumzia : Mipaka katika mabadiliko: Ulaya na Uislamu baada ya mashambulio ya kigaidi ya Paris. Kati ya watakaotoa mchango katika mkutano huu ni Askofu Mkuu wa Milan, Kardinali Angelo Scola. Wengine watakaotoa mchango ni Profesa Abdelmajid Charfi, Mkuu wa zamani wa Kitivo cha Sayansi ya Binadamu, katika Chuo Kikuu La Manouba, Tunis, pia Profesa Henry Laurens wa Chuo de France cha Paris, na Profesa Riccardo Redaelli wa Chuo Kikuu Katoliki cha Moyo Mtakatifu cha Milan.
Mjadala utazinduliwa na Profesa Franco Anelli, gombera wa Chuo Kikuu Katoliki, na mwanasheria Giuseppe Guzzetti, mwenyekiti wa Shirika la Cariplo. Mjadala wa mahusiano kati ya Ulaya na ulimwengu wa Kiislamu, unalenga hasa kutafakari na kutoa jibu la pamoja kwa haraka zaidi, baada ya mashambulizi ya kutisha huko Paris.
All the contents on this site are copyrighted ©. |