2015-11-27 09:48:00

Baba Mtakatifu Francisko anataka kuimarisha Uekumene wa damu!


Mama Kanisa anaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa uwepo na ushuhuda wa Mashahidi wa Uganda, waliotangazwa kuwa Watakatifu takribani miaka 50 iliyopita. Hili ni kundi la mashuhuda 22 wa imani, waliokuwa wanafanya kazi zao kwenye himaya ya Mfalme wa Buganda. Watu hawa wa kawaida kabisa, wakapoikea na kuikumbatia imani ya Kikristo kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Wamissionari wa Afrika.

Mashuhuda hawa wa imani waliuwawa kikatili wakati wa utawala wa Mfalme Mwanga wa pili aliyetawala kati ya mwaka 1884 hadi mwaka 1903. Historia inaonesha kwamba, mashuhuda wa imani nchini Uganda waliuwawa kati ya tarehe 15 Novemba 1885 na tarehe 27 Januari 1887. Kutokana na ushuhuda thabiti wa imani, kiasi cha kuwa tayari kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, Papa Benedikto XV, tarehe 6 Juni 1920 akawatangaza kuwa ni Wenyeheri na tarehe 8 Oktoba 1964 wakatangazwa kuwa Watakatifu na Papa Paulo VI.

Mwenyeheri Paulo VI alitekeleza dhamana hii katika hija yake ya kitume Barani Afrika na kumtangaza Karoli Lwanga kuwa ni mfano bora wa kuigwa kati ya mashuhuda wote wa imani, kwani alisimama kidete bila woga wala makunyanzi kushuhudia imani yake, akawatia shime ndugu zake ili kukabiliana na mateso kwa ujasiri na imani thabiti. Leo hii Namgongo ni kati ya Madhabahu maarufu sana ya mashuhuda wa imani Barani Afrika. Kila mwaka waamini na watu wenye mapenzi mema wanamiminika Namgongo kwenda kutoa heshima kwa mashuhuda hawa wa imani. Itakumbukwa kwamba, hili ni kundi kubwa kutoka Barani Afrika kuwahi kutangazwa na Mama Kanisa kuwa ni watakatifu. Mashahidi wa Uganda wanakumbukwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Juni, kadiri ya Kalenda ya Kanisa Katoliki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.