2015-11-26 17:09:00

Tunzeni mazingira, mipango miji ipambane na umaskini na mwanadamu aheshimiwe!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Kenya, Alhamisi tarehe 26 Novemba 2015 ametembelea Ofisi za Umoja wa Mataifa na kukutana na viongozi pamoja na wafanyakazi wa Ofisi ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa pamoja na Makazi ya watu. Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kulinda na kutunza maliasili; uwajibikaji wa pamoja sanjari na ukuzaji wa utamaduni wa hifadhi bora ya mazingira. Amegusia ukuaji wa miji na mapambano dhidi ya umaskini na hali ya kuwatenga watu inayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia.

Kwa maneno machache, Baba Mtakatifu Francisko ametoa muhtasari wa Waraka wake juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si, ameangalia kwa kina na mapana mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP21 utakaofanyika Paris, Ufaransa pamoja na mkutano wa kimataifa juu ya makazi ya watu unaotarajiwa kufanyika huko Quito, Mwezi Oktoba 2016 pamoja na mkutano wa Biashara kimataifa unaotarajiwa kufanyika Jijini Nairobi hivi karibuni.

Baba Mtakatifu anazihamasisha Jumuiya za Kimataifa na Mashirika ya Kiserikali na watu binafsi kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira kwa kuweka sheria na sera makini pamoja na kuzishinikiza Serikali kutekeleza dhamana yake barabara, ili kulinda na kutunza mazingira pamoja na maliasili. Baba Mtakatifu anasema, litakuwa ni jambo la kusikitisha sana ikiwa kama mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utashindwa kupata muafaka wa pamoja kwa ajili ya mafao ya wengi na badala yake kuyaweka mafao haya rehani kwa mikono ya watu binafsi, ili kulinda miradi yao binafsi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema mazingira ni fao la wengi na kwamba, mabadiliko ya tabianchi ni tatizo la kimataifa ambalo linahitaji kupata jibu muafaka kutoka katika jamii inayojali haki msingi kwa maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi. Hapa kuna haja ya kuwa na sera na taratibu mpya katika masuala ya kisiasa na kiuchumi ili kurekebisha mifumo duni ya maendeleo ambayo imepitwa na wakati. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutekeleza maamuzi yake kwa vitendo kwani watu wamechoshwa na maneno matupu wanataka kuona vitendo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira utakuwa ni chachu ya mabadiliko kwa kujikita katika misingi ya mshikamano, haki, usawa, ushiriki kwa kujielekeza zaidi katika mambo msingi matatu yaani: kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi; kukoleza mapambano dhidi ya umaskini pamoja na kulinda utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu wa binadamu. Sera na mikakati ya elimu ilenge katika mchakato wa utamaduni mpya wa utunzaji unaojikita katika medani mbali mbali za maisha bila kumezwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kwani matokeo yake ni kuibuka kwa kasi ya ajabu utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; kazi za suluba na ukahaba. Kuna ongezeko kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya maisha yao kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hawa ni watu ambao wanakufa maji kila siku na Jumuiya ya Kimataifa haina haki kufumbia macho mahangaiko yao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukuaji wa miji hauna budi kwenda sanjari na mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani, ili kuboresha makazi ya watu, yanayoheshimu na kuthamini utu wa binadamu, umoja na mafungamano ya kijamii. Vinginevyo miji itakuwa ni viwanja vya fujo na kinzani; maduka ya biashara haramu ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; watu kupoteza utambulisho wao kiasi cha kukosa dira na mwelekeo. Kuwepo na mipango mizuri ya makazi ya watu, kwa kuacha maeneo ya wazi ili kujenga mazingira bora ya maisha kwa watu wengi zaidi.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mkutano wa Makazi ya Watu utakaofanyika mwezi Oktoba 2016 utasaidia kubainisha sera makini za mipango miji. Mwishoni, Baba Mtakatifu anaonesha matumaini kwa mkutano wa biashara kimataifa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni Jijini Nairobi utajikita katika huduma kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote; maendeleo endelevu pamoja na kuwajali maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waonje ushirikiano na kupata huduma ya afya, ambayo Kanisa Katoliki limekuwa ni mdau mkuu. Huduma hii iwe ni kwa ajili ya wote na wala si kwa watu wachache! Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza kilio cha watu, lakini zaidi watu kutoka Barani Afrika, sehemu ambayo rasilimali na utajiri wake unatumiwa kwa mafao ya watu wachache, huku wengi wakitumbukizwa katika baa la umaskini!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.