2015-11-26 17:22:00

Mkileta utani nitakwenda Bangui kwa Parachuti!


Baba Mtakatifu Francisko wakati akiwa njiani kuelekea nchini Kenya kwa ajili ya hija yake ya kitume Barani Afrika, ndani ya ndege alipata nafasi ya kusalimiana na waandishi wa habari 74 kutoka katika mataifa mbali mbali ambao wako kwenye msafara wake ili kuhakikisha kwamba, watu wengi wanapata walau kujua yale ambayo yanaendelea kujiri wakati wa hija hii ya kitume Barani Afrika. Katika msafara huu kulikuwepo na waandishi wa habari wanne kutoka Kenya !

Baba Mtakatifu alipewa zawadi ya kitabu cha wafungwa kutoka Argentina na kusema kwamba, kwa hakika kati yao kuna marafiki zake.  Alipoulizwa ikiwa kama alikuwa anaogopa mashambulizi ya kigaidi, Baba Mtakatifu alikaza kusema, yeye alikuwa anaogopa zaidi mbu kuliko hata mabomu ya kujitoa mhanga! Baba Mtakatifu alisalimiana na wafanyakazi na wahudumu wote wa Ndege iliyowabeba kuelekea Nairobi, Kenya. Rubani wa ndege hiyo amemhakikishia Baba Mtakatifu kwamba, atampeleka pia Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, lakini Baba Mtakatifu akaonya kwamba, ikiwa kama atashindwa kutekeleza ahadi yake, basi ampatie parachuti, yeye atashuka bila wasi wasi ili kukutana na kuzungumza na Familia ya Mungu Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Akiwa nchini Uganda, Baba Mtakatifu anataka kutoa heshima yake kwa mashuhuda wa imani wanaoendeleza mchakato wa Uekumene wa damu na kwamba, hija yake ya kitume nchini Uganda inaongozwa na kauli mbiu, “Mtakuwa ni mashahidi wangu”. Hija ya Baba Mtakatifu inalenga kuwaimarisha waamini wote Barani Afrika ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Wawe ni wajumbe wa Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka mioyo, tayari kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali, kielelezo cha utandawazi wa mshikamano.

Padre Federico Lombardi amesema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko siku moja kabla ya kuondoka na kuanza safari yake Barani Afrika, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma ili kusali na kujikabidhisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu akizungumza na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake amewaomba kusaidia kuwahabarisha watu mambo msingi ili hija hii ya kitume iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Yeye anakwenda Afrika ili kukutana na ndugu zake katika Kristo kwa furaha na matumaini makubwa.

Baba Mtakatifu Francisko alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Jijini Nairobi amepokewa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pamoja na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya waliokuwa wameandamana na baadhi ya viongozi wa Serikali na Kanisa. Baba Mtakatifu aliweka sahihi kwenye kitabu cha wageni maarufu nchini Kenya na kuandika sala ya kuiombea Kenya baraka, amani na furaha kwa watoto wake wote na baadaye alipokuwa Ikulu ya Kenya, alipanda mti alama ya ustawi na maendeleo kwa wananchi wa Kenya ambao wana utamaduni wa kupanda na kutunza miti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.