2015-11-26 16:58:00

Asante sana Baba Mtakatifu Francisko! Makali yako tumeyaona!


Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Alhamisi tarehe 26 Novemba 2015, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa uwepo wake na kwa kuwaimarisha ndugu zake katika imani; kwa kuwafundisha na kushuhudia imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na kwamba, amekuwa kweli ni nguzo ya umoja na mshikamano wa Kikanisa na rasimali rejea kwa changamoto ambazo zinamwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Njue ameishukuru Serikali ya Kenya kwa kuonesha ushirikiano na mshikamano katika maandalizi  na hatimaye, mapokezi ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya. Amewashukuru wajumbe kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Mashariki na Kati, AMECEA kwa kuonesha umoja na mshikamano wa Kanisa bila kuisahau Familia ya Mungu nchini Kenya iliyojisadaka kwa hali na mali ili kufanikisha hija ya Baba Mtakatifu nchini Kenya.

Kardinali Njue amewakumbuka na kuwashukuru Wasamaria wema waliochangia kwa hali na mali ili kufanikisha hija hii ya kitume bila kuwasahau waamini wa dini mbali mbali pamoja na watu wote wenye mapenzi mema waliohudhuria katika Ibada hii ya Misa Takatifu. Kwa wote hawa anawaombea umoja, amani na uhuru ili viweze kukaa na kudumu katika maisha yao yote! Familia ya Mungu anasema Kardinali Njue, kweli imeonesha upendo na umoja kwa kusafiri mwendo mrefu ili kwenda Nairobi kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu. Hiki kiwe ni kielelezo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa kutambua kwamba wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.