2015-11-26 16:41:00

Ambateni Injili ya familia; jikiteni kwa Yesu, ili kuwa Wamissionari


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 26 Novemba 2015 mara baada ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa dini nchini Kenya, amepata nafasi ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Chuo kikuu cha Nairobi kwa ajili ya Uinjilishaji wa watu! Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kuambata Injili ya familia kadiri ya mpango wa Mungu; changamoto kwa waamini kusimika maisha yao juu ya Mwamba thabiti ambao ni Kristo Yesu pamoja na kuhakikisha kwamba, kweli waamini wanakuwa ni Wamissionari tayari kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa njia ya uhalisia wa maisha yao!

Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa wa waamini kutoka ndani na nje ya Jiji la Nairobi na kwamba, hawa waliohubiriwa Neno la Mungu wanafanyika kuwa ni sehemu ya Familia ya Mungu na Kanisa la Kristo, kama ilivyo hata kwa waamini kutoka nchini Kenya. Familia nchini zimebarikiwa kwa kuwa zinajikita katika tunu bora za maisha, kwa kuwaheshimu na kuwaenzi wazee pamoja na kuwapokea watoto kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Imani tendaji inayobubujika kutoka katika Neno la Mungu, iwasaidie waamini kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya familia, kwa kuwapokea watoto na kuwalea; kwa kulinda utu na heshima ya binadamu, kwani wote wanaunda familia ya binadamu!

Utii kwa Neno la Mungu anakaza kusema Baba Mtakatifu iwe ni nafasi ya kwa watu kuondokana na mila na tamaduni zinazowanyanyasa na kuwabeza wanawake au kukumbatia utamaduni wa kifo. Waamini wanahamasishwa kuwa Wasamaria wema kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze kuonja upendo wa Mungu na nguvu ya maji ya Roho Mtakatifu ili kulainisha ukavu na jangwa katika mioyo ya watu linalosababishwa na utamaduni wa kupenda mno malimwengu na kuwabeza wengine.

Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu; wanaimarishwa kwa mapaji ya Roho Mtakatifu wanapokea Sakramenti ya Kipaimara inayowakirimia furaha na nguvu ya maisha ya kiroho; kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wanashiriki Mwili na Damu yake azizi kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Hizi ni zawadi muhimu sana katika ustawi na maisha ya Kanisa na Kenya katika ujumla wake, tayari kujisadaka kwa jili ya upendo, huruma na ukarimu dhidi ya ulimwengu ambao umegubikwa kwa ubinafsi, dhambi na migawanyiko. Kwa njia ya imani, Mwenyezi Mungu anawajalia waja wake uwezo wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi yao kwa kujikita katika: amani, utulivu na mshikamano wa kidugu.

Hizi ni zawadi ambayo vijana wa kizazi kipya wanapaswa kushirikishwa kikamilifu Barani Afrika. Chuo kikuu ni mahali ambapo akili na mioyo ya vijana wa kizazi kipya inaundwa, changamoto kwa walezi kuhakikisha kwamba, wanawasaidia vijana kupata tunu msingi za maisha ya Kiafrika, hekima na ukweli wa Neno la Mungu, ili kuwa ni dira na mwongozo wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, utu, heshima pamoja na kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wapewe kipaumbele cha pekee, waamini wawe na ujasiri wa kukataa maamuzi mbele na ubaguzi, kwani mambo haya ni kinyume kabisa cha Mwenyezi Mungu.

Changamoto kubwa kwa waamini ni kuyasimika maisha yao juu ya mwamba thabiti ambao ni Yesu Kristo, Mkombozi wa dunia; tayari kutoka kimasomaso kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji unaojikita katika ukweli, wema, uzuri na nguvu ya Injili inayoleta mabadiliko katika maisha ya mwamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa ni vyombo vya neema ya Mungu inayobubujika kutoka katika huruma yake, upole na ukweli msingi imara wa maisha ya mwamini.

Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni wafuasi na wamissionari wanaohamasishwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao yaliyoshuhudiwa na Kristo Yesu ambaye ni chemchemi ya uhuru na amani. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kuwataka waamini kujenga maisha na familia zao katika Kristo Yesu ambaye ni njia ya wema na huruma kwa maisha yao yote. Mwenyezi Mungu awabariki na kuwalinda wananchi wote wa Kenya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.