2015-11-25 16:31:00

Wananchi wa kitongoji cha Kangemi wana msubiri Papa Francisko kati yao!


Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akitoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwani hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Wakati wa hija yake ya kitume nchini Kenya kuanzia tarehe 25- 27 Novemba pamoja na mambo mengine yote, lakini atapata nafasi ya kutembelea na kuzungumza na wananchi wanaoishi katika kitongoji cha Kangemi, nje kidogo ya Jiji la Nairobi.  Haya ni makazi yasiyo rasmi ambayo yanagubikwa na umaskini mkubwa wa hali na kipato.

Takwimu zinaonesha kwamba, maeneo kama haya Jijini Nairobi yako saba, lakini kwa wakati Baba Mtakatifu anatembelea Parokia ya Mtakatifu Yosefu iliyoko kwenye Kitongoji cha Kangemi. Padre Melchior Marandu, SJ ni kati ya Mapadre wanaotoa huduma ya kichungaji katika kitongoji hiki chenye mazingira hatarishi. Anasema, wanayo furaja kubwa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko. Tayari wamejiandaa kiroho na kimwili ili kumpokea Baba Mtakatifu aweze kuwapatia neema na baraka.

Parokia inaishukuru Serikali ya Kenya kwa ushirikiano mkubwa uliojionesha hadi kufanikisha maandalizi muhimu na sasa wako tayari kumpokea mgeni wao na akipenda anaweza hata kupata eneo la kujibanza, ili aweze kuendelea kuwaimarisha ndugu zake katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Wanawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali ili kumwombea Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, aendelee kuwajali na kuwagusa maskini, ili hata viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waweze kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.