2015-11-25 08:37:00

Ujio wa Baba Mtakatifu Francisko ni alama ya matumaini Barani Afrika!


Kardinali John Njue,Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anasema, ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya ni sauti ya kinabii inayopenda kuhamasisha wanasiasa na waamini wa dini mbali mbali kujikita katika mchakato wa maridhiano ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Kuna mabadiliko makubwa yaliyokwisha kutoka nchini Kenya tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Kenya kwa nyakati tofauti, takribani miaka ishirini iliyopita.

Baba Mtakatifu Francisko anawatembelea Wakenya ambao kwa sasa ni millioni 44 wanaotoka katika makabila 42. Kati yao kuna Waamini Wakatoliki wapatao millioni kumi na nne wanaohudumiwa katika majimbo makuu manne yanayounda majimbo 24 ya Kanisa Katoliki nchini Kenya.  Yote haya ni matunda ya changamoto iliyotolewa na Papa Pio IX katika Waraka wake wa kitume, “Zawadi ya imani” “Fidei Donum”,  uliowahamasisha Wamissionari wengi kujisadaka kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu Barani Afrika na matunda ya sadaka hii ni Mwenyeheri Sr. Irene Stephane, aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 23 Mei 2015 katika Jimbo kuu la Nyeri, Kenya.

Mwenyeheri Irene anafahamika na wengi kama “Nyaatha” maana yake, “Mwenye huruma”, aliyejisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; akawajengea watu imani na matumaini kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa linaendeleza mchakato wa kutaka kumtangaza Mtumishi wa Mungu Kardinali Maurice Otunga kuwa ni Mwenyeheri. Huyu ni kiongozi wa Kanisa aliyeonesha unyenyekevu mkuu, akajisadaka bila ya kujibakiza katika huduma za kichungaji pamoja na kuwakumbatia maskini, ili waonje huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Mtumishi wa Mungu Kardinali Otunga alikuwa na upendo wa hali ya juu kwa Mungu, akaonesha heshima kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Yote haya ni matunda ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa Katoliki nchini Kenya linaendeleza mchakato wa mabadiliko kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Kenya kwa njia ya huduma makini; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima, haki na uhuru wa wananchi wote wa Kenya pasi na ubaguzi.

Kardinali Njue anasema, Familia ya Mungu nchini Kenya inasubiri kwa hamu ujumbe na changamoto kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati huu Kenya inapoendelea kukabiliana na utandawazi ambao unapelekea hata kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya Kiafrika, kanuni maadili na utu wema. Bado kuna idadi kubwa ya wananchi wa Kenya wanaoogelea katika kashfa ya umaskini; kuna ubaguzi wa kidini, kisiasa na kikabila; saratani ya rushwa bado haijapata tiba muafaka; changamoto ambazo Kanisa nchini Kenya imezivalia njuga.

Maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Kenya unaendelea kushamiri kwa kuwa na idadi kubwa ya miito ya Kipadre na kitawa, leo hii Kenya ina wamissionari walioenea sehemu mbali mbali za dunia, changamoto ni kuendelea kumpatia Kristo kipaumbele cha kwanza kwa kujikita katika ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika huduma makini kwa Familia ya Mungu nchini Kenya. Kanisa liko mstari wa mbele kuendeleza utume kwa vijana na watoto.

Kenya bado inawakumbuka na kuwalilia wanafunzi 147 waliouwawa kikatili tarehe 4 Aprili 2015 kwenye Chuo Kikuu cha Garissa, hapana shaka kwamba, wanafunzi hawa watakumbukwa na Baba Mtakatifu wakat iwa hija yake nchini Kenya. Iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Hija ya Baba Mtakatifu itaimarisha mkakati wa kupambana na vitendo vya kigaidi, ili kujenga na kuimarisha maridhiano, haki na amani kati ya wananchi wote wa Kenya. Hii ni zawadi kwa Kanisa Barani Afrika kwani Baba Mtakatifu anataka kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.