2015-11-25 09:26:00

Toba na wongofu wa ndani muhimu ili kuambata upendo na huruma ya Mungu


Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo ni alama ya matumaini na baraka kwa familia ya Mungu nchini humo inayotaka kuondokana na vitisho vya vita na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia ambayo yamedumu nchini humo kwa takribani miaka mitatu sasa pasi na suluhu ya amani. Wananchi wanataka kujenga msingi wa haki, amani na utulivu, tayari kuanza  ukurasa mpya wa maisha baada ya kukimbilia msituni na kuishi huko kwa zaidi ya miaka mitatu!

Askofu mkuu Nzapalainga anakaza kusema, umaskini, magonjwa na mahangaiko ya wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati pamoja na kilio chao kimemfikia Baba Mtakatifu Francisko na sasa anakuja kuwafariji, tayari kuanza mchakato wa upatanisho unaopata chimbuko lake kutoka katika undani wa mioyo ya watu. Mara kwa mara Baba Mtakatifu amekuwa akiwakumbuka na kusali kwa ajili ya Familia ya Mungu nchini Afrika ya Kati, alama ya upendo na mshikamano wa kibaba kwa watu wanaoteseka na kunyanyasika.

Kwa kweli wananchi wanakosa maneno ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu na kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuonesha moyo wa ujasiri na upendo wa kibaba, kwa kuwachagua maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kuwa ni sehemu ya vipaumbele vya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hja ya Baba Mtakatifu ni habari njema kwa Familia yote ya Mungu nchini Afrika ya Kati na wengi wanamwona kuwa kweli ni mjumbe wa amani “Watokua ti siriri”. Kuna wasi wasi wa usalama, lakini wananchi wengi wanaendelea kuonesha utulivu na kumsubiri Baba Mtakatifu kwa imani na matumaini makubwa.

Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ni maskini na wala Baba Mtakatifu Francisko hatarajii kuona makubwa, lakini anakuja kati yao ili kupandikiza mbegu ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu, tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha na kuachana na mzunguko wa vita na kinzani za kijamii ambazo hazina mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi.

Hija ya Baba Mtakatifu inalenga kuwainua wakimbizi na wahamiaji kutoka katika unyonge wao, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini. Baba Mtakatifu ni mjumbe wa Mungu na kwa njia yake, Mwenyezi Mungu ataweza kuzungumza na kugusa mioyo ya wengi huko Afrika ya Kati. Kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Afrika ya kati ni “Tuvuke upande wa pili wa mto”. Baba Mtakatifu anataka kuivusha Familia ya Mungu Afrika ya Kati, ili kuingia katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kufungua lango la Kanisa kuu la Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili, tayari waamini kuambata upendo na huruma ya Mungu inayojikita katika toba, wongofu na upatanisho. Ni wakati wa kuondokana na chuki, hasira na hali ya kulipizana kisasi na badla yake kuambata neema na huruma ya Mungu, kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu anataka kuwainua na kuwakweza wananchi wa Afrika ya Kati ili kuondokana na unyonge wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.