2015-11-25 08:53:00

Familia ya Mungu nchini Uganda inachangamotishwa kuwa ni mashuhuda wa imani


Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala Uganda anasema, Familia ya Mungu nchini Uganda inayofuraha na heshima kubwa kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika anayekuja kuwashirikisha ndugu zake ujumbe wa: amani, huruma na matumaini, tayari kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushuhudia imani yao kwa Kristo Yes una Kanisa lake, kwani wote wanaalikwa kuwa ni mashahidi wake, kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Uganda.

Baba Mtakatifu Francisko anakwenda Uganda ili kuwaimaaisha ndugu zake katika imani, dhamana ambayo Yesu Kristo alimkabidhi Mtakatifu Petro, kumbe hii ni changamkoto kwa Familia ya Mungu nchini Uganda kuwa kweli ni mashuhuda wa mwanga wa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu anataka kugusa na kuonja maisha ya Familia ya Mungu nchini Uganda. Uganda imebahatika kuwa na mashuhuda wengi wa imani waliotangazwa na Mama Kanisa kuwa ni watakatifu. Ikabahatika kuwa na Wakleri wa kwanza wazalendo kunako mwaka 1913 na kunako Mwaka 1939 Uganda ikapata Askofu wake wa kwanza.

Askofu mkuu Lwanga anakaza kusema, Uganda imebahatika kuwapokea na kuwakaribisha Mapapa watatu, yaani: Mwenyeheri Paulo VI, Mtakatifu Yohane Paulo II na kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko, changamoto ya kutambua na kuthamini mchango wa Kanisa Barani Afrika katika mchakato wa Uinjilishaji miongoni mwa Familia ya Mungu Barani Afrika. Uganda ilibahatika kuwa ni kati ya nchi za kwanza kwanza Barani Afrika kuwa na Makatekista, ambao wengi wao walikufa kifodini kwa kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Uganda bado ina madonda ya vita, chuki na utengano kutokana na uasi uliofanywa na Joseph Kony na jeshi lake ya waasi wa Uganda. Familia ya Mungu nchini Uganda inataka kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu, kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kujisadaka kwa ajili ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha; uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia inajengwa katika msingi wa mahusiano thabiti kati ya bwana na bibi na wala si vinginevyo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.