2015-11-23 15:25:00

Vatican inalaani kwa nguvu zote vitendo vya kigaidi!


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wananchi wote wa Mali walioguswa na kutikishwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyojitokeza nchini humo hivi karibuni na kupelekea watu 21 kupoteza maisha na mateka 19 kuachiliwa baadaye. Kutokana na shambulizi hili, Serikali ya Mali ikatangaza siku 10 ya hali ya hatari nchini Mali.

Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Jean Zerbo wa Jimbo kuu la Bamako, Mali, anapenda kuwafariji na kuwaweka wote walioguswa na msiba huu mkubwa chini ya ulinzi na faraja ya Mwenyezi Mungu na wale waliopata majeraha waweze kupona haraka. Baba Mtakatifu analaani kwa nguvu zote vitendo vya kigaidi na anamwomba Mwenyezi Mungu awajalie moyo wa toba, wongofu wa ndani na amani ya kweli, watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kigaidi. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, anawapatia wale wote walioguswa na msiba huu baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.