2015-11-23 10:39:00

Tuvuke upande wa pili wa mto! Tufungue lango la Jubilei ya huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa Familia ya Mungu Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wakati huu anapojiandaa kutembelea Barani Afrika anasema, anapenda kuwashirikisha wananchi wote wa Afrika ya Kati, furaha yake anapotembelea kwa mara ya kwanza Bara la Afrika, lenye uzuri wa kuvutia, lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, watu na tamaduni. Ni matumaini yake kwamba, hija yake ya kichungaji itamwezesha kugundua utajiri mkubwa kutoka Barani Afrika utakaoboreshwa zaidi kwa kukutana na watu mbali mbali.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa muda mrefu inakabiliwa na mgogoro wa kivita na ukosefu wa usalama hali ambayo inapelekea mateso makubwa kwa watu wengi wasiokuwa na hatia. Lengo la hija yake nchini humo kwa jina la Yesu anasema Baba Mtakatifu ni kuwafariji na kuwapatia matumaini mapya. Ni matumaini yake kwamba, hija yake ya kitume nchini humo itachangia kuponya madonda ya utengano, ili kujenga na kudumisha amani na utulivu kwa wananchi wote wa Afrika ya Kati.

Kauli mbiu ya hija hii ya kichungaji ni “Tuvuke upande wa pili wa mto!”. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya za Kikristo huko Afrika ya Kati kuwa na ujasiri kwa kujikita katika mchakato wa kupyaisha upya mahusiano yao na Mungu pamoja na jirani, ili kujenga dunia inayosimikwa katika haki na udugu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, atakuwa na furaha ya pekee kabisa wakati atakapofungua lango la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, kielelezo makini cha neema ya Mungu inayojikita katika msamaha kwa kupokea na kutoa msamaha sanjari na kupyaisha fadhila ya upendo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, anakuja kati yao kama mjumbe wa amani, tayari kusaidia mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kukuza na kudumisha amani na utulivu, kwani hili ni jambo linalowezakana kwani wote ni watoto wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumkumbuka na kumshindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na kwamba, anawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.