2015-11-23 15:02:00

Mwaka wa Watawa Duniani: Uzito wa maisha ya kitawa na utume wake!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Tukingali ndani ya Mwaka wa Watawa Duniani, tunaendelea kujulishana machache na kwa uchache sana yahusuyo maisha ya kitawa. Katika kipindi kilichopita, tuliangazia juu ya uzito na thamani ya maisha ya kitawa katika Kanisa na katika ulimwengu kwa ujumla. Uzito wa maisha ya kitawa tunaweza kuuona nyanja kuu nne kama ifuatavyo: Mosi, tunautazama ukuu wa maisha ya kitawa katika asili yake, yaani ni Mungu ndiye mwenye kuita, hivyo utawa ni wito mtakatifu sio tu mfumo wa maisha.

Na Mwenyezi Mungu humwita mtu kwa namna ya pekee, kwa wakati mwafaka na kwa lengo maalumu, na kwa vigezo vyake Mungu mwenyewe. Na huenda akamwitwa mtu na kumtuma kwa watu maalumu, kama ilivyokuwa kwa manabii wa kale. Hali kadhalika mtawa, ni chombo cha Mungu, kwa ajili ya kutimiza mapenzi ya Mungu, namna atakavyo Mungu mwenyewe ndani ya Kanisa, kadiri ya Karama ya shirika na miongozo ya Mama Kanisa Mtakatifu.

Pili, tunautazama ukuu wa maisha ya kitawa  katika vifungo vyake. Mtu akisha kuitwa na Mungu katika wito wa kitawa, haitoshi tu kuitika na kuishi katika jumuiya au pekee yake au katika mfumo wowote wa kitawa, bali ni lazima kabisa, huyu aliyeitwa, athibitishe kuitwa kwake, kwa kujitoa kikamilifu kwa Mungu kwa vifungo maalumu;  iwe ni nadhiri, ahadi au aina nyingine ya muungano mtakatifu, kadiri ya utaratibu wa Shirika lake au mwongozo uliowekwa na Kanisa. Kwa njia ya hizo nadhiri au ahadi, mtawa anayamimina maisha yake yote kwa ajili ya utumishi kwa Mungu, ndani ya Kanisa na pamoja na Kanisa, ili kuendeleza kazi ya ukombozi wa Mwanadamu kiroho na Kimwili. Watawa wa Bwana, wameitwa – wametwaliwa na wao wenyewe wamejiweka wakfu kwa Mungu, wamemwahidia Mungu kwa kiapo, katika Ufukara Mtakatifu, Useja mtakatifu pamoja na Utii mnyoofu. Ni kwa njia hiyo wanajiambua na malimwengu yote, ili wabaki huru na safi kwa ajili ya Mungu tu.

Tatu, tunautazama ukuu wa maisha ya kitawa katika huduma zake. Utawa ni wito wa utumishi. Yeyote aliyeitwa kuwa mtawa, mmoja kwa mmoja bila kupindisha shingo, ameitwa kujisadaka, kujimega, kujimaliza kwa ajili ya Mungu, kwa njia ya huduma mbalimbali za kiroho na kimwili. Tukienda ndani kidogo tunaweza kusema hivi: Watawa wa Yesu, wanaoyaishi mashauri ya Kiinjili, huku wakiifafanua Injili ya Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao na huduma zao, hao ni ishara ya Kristo Yesu, anayeendelea kujimega na kujitoa kwa ajili ya wokovu wa wengi. Hivyo huduma za Watawa sio tu kazi kama za watu wa mshahara, bali zina uwakfu ndani mwake. Kwa sababu ni huduma zinazolenga kuendeleza kazi zilezile za Yesu kati ya watu.

Kadiri ya maratibisho ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican, maisha ya kitawa yanaalikwa zaidi kujituma kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, kwa njia ya huduma za watawa kwa mwanadamu, mwanadamu anasindikizwa katika hija yake ya hapa duniani ya kumwendea Mungu. Ni hapo ndipo twaweza kusema, maisha na huduma za watawa kwetu sisi, ni ishara ya wema na uwepo wa Mungu anayetenda kazi kati ya watu wake. Ni katika mantiki hii mara mmoja tulisema, watawa ni vidole vya Kristo, wanaendeleza huduma zilezile za Kristo kwa wanadamu.  Wametwaliwa, wamebarikiwa, nao wakajiweka wakfu, na sasa kwa huduma zao wanaendelea kujimega. Sadaka hiyo ya maisha ya kitawa.

Nne, tunautazama ukuu wa maisha ya Kitawa katika fumbo la uwingi wa mashirika. Roho Mtakatifu nyakati mbalimbali anawavuvia watu kuanzisha mashirika ya kitawa, kwa lengo la kujibu mahitaji maalumu ndani ya Kanisa kadiri Roho mwenyewe apendavyo. Injili ya Kristo ni ileile mmoja na ya daima, kwani Kristo ni yuleyule jana leo na daima. Lakini watawa wanaoifafanua Injili ya Kristo katika matendo halisia ya maishani, ni wengi sana. Uwingi wa mashirika ya Kitawa ndani ya Kanisa, ni fumbo la Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa nyakati mbalimbali. Kwa fumbo hilo ndiyo maana twaweza kuona kuwa, hata katika mashirika yale makongwe, bado roho wa Bwana anaweza kuingia na kuleta mageuzi makubwa yanayowapeleka katika lengo maalumu, iwe ni kwa faida ya Shirika lenyewe au kwa faida ya Kanisa zima la Mungu.

Kwa vigezo hivyo vinne, tunaona wazi maisha ya Kitawa si mradi wa mwanadamu, ni kazi ya Mungu mwenyewe. Mungu mwenyewe ameridhia kwamba baadhi watengwe kwa kazi maalumu. Watawa wametengwa na Mungu kwa kazi maalumu. Ni kwa uzito huo na ukuu huo, Kanisa linajivunia maisha ya Kitawa na huduma zake kama ishara hai ya kazi ya Mungu inayoendelea kutendeka. Tunasema tena, kwa kuenzi zawadi hii ya Mungu ndani ya Kanisa, Baba Mtakatifu anatualika sote pamoja, kwa mwaka huu, tusali kumshukuru Mungu kwa neema ya Maisha ya Kitawa na tuwaombee watawa wetu katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Swali la msingi: Je, Maisha ya kitawa yalianza lini hasa? Tukumbuke kwamba, maisha ya kitawa yapo katika dini mbalimbali. Sisi hapa tunaongelea utawa katika Kanisa letu, Mmoja Takatifu Katoliki la Mitume. Hapa tutazungumzia aina zake tofauti zilizojitokeza katika Kanisa  kadiri ya wakati na mahali mbalimbali ambapo Roho Mtakatifu aliwakirimia watu wake wajitoe kabisa kwa ufalme wa Mungu.  Kama tulivyowahi kusema; Utawa ni  jina hilo linalojumuisha maisha ya aina nyingi yanayomshuhudia Kristo katika sifa na kazi zake mbalimbali.

Mwanzoni kabisa kufuatana na mifano ya Bikira Maria na hasa na maisha ya Yesu mwenyewe, kuna wanaume na wanawake   waliojinyima ndoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu, kama vile mabinti wanne wa shemasi Filipo waliokuwa mabikira na manabii (Mdo. 21:9). Mtume Paulo naye akitafakari ubora wa aina hiyo ya maisha aliwahimiza Wakristo wanaoweza kuyaambata maisha hayo na wafanye hivyo kama alivyofanya mwenyewe kufuatana na shauri la Bwana (1Kor. 7:25-34).

Katika kipindi cha Mababa wa Kanisa, kuanzia Karne ya I tunasoma sifa za watu wa toba wanaozunguka huko na huko  ili kuhubiri habari njema ya Ufalme wa Mungu. Na pi tunaona habari za mabikira ambao utakatifu wao unaonyeshwa kama alama ya ubora wa Ukristo juu ya ulimwengu wa anasa unaoliudhi Kanisa. Polepole, Mabikira hao walianza kuorodheshwa na kukubaliwa na Askofu na kukusanywa katika jumuia (utawa wa mabikira). Ilitokea vilevile kwa wanaume wa toba walioanzisha miundo kamili kuliko juhudi za nyumbani mwao, wakishika ufukara wa hiari, mafungo, kujinyima vyakula mbalimbali, kukesha usiku huku wakisali kwa kuimba Zaburi, kufanya tafakari na kusali kwa moyo, huku wakiyasimika maisha yao katika misingi ya Injili ya Kristo. Aina hiyo ya maisha na sifa zake  zimekua ndani ya Kanisa kwa vipindi mbalimbali hadi kufikia nyakati zetu hizi. Juma lijalo tutaviangazia vipindi mbalimbali vya ukuaji wa utawa na tabia zake.

Kutoka Studio za Radio vatican ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB, Mtawa wa Shirika la Mtakatifu Benedikto kutoka Abais ya Roho Mtakatifu-Mvimwa, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.