2015-11-23 08:22:00

Mapadre ni wahudumu wa Mafumbo Matakatifu ya Kanisa!


Katika kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Matamko kuhusu Seminari “Optatam totius” na Wito wa Mapadre “Presbyterorum ordinis”, imekuwa ni nafasi murua kabisa kwa Baraza la Kipapa la Wakleri kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko hapa mjini Roma kufanya kongamano ambalo limepembua kwa kina na mapana kuhusu wito na maisha ya Kipadre; utambulisho na utume wa Mapadre.

Kongamano hili ambalo limefanyika hivi karibuni, liliongozwa na kauli mbiu “Wito, majiundo na utume; hija ya ufuasi wa Kipadre kadiri ya Matamko ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Seminari na Wito wa Mapadre. Wajumbe mbali mbali walipata nafasi ya kuweza kuzama tena katika hazina ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kuangalia umuhimu wa nyaraka hizi katika maisha na utume wa Mapadre katika ulimwengu mamboleo, lakini zaidi kwa kujikita katika imani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, kiini cha Habari Njema ya Wokovu na kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake, tayari kuwaonjesha uhuru na hatimaye kuweza kukutana naye katika hija yao ya maisha!

Haya yamezungumzwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati akichangia tafakari kuhusu Nyaraka za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu uhamasishaji wa miito na majiundo makini ya Mapadre, ili kuwawezesha kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa, kwa kumfuasa Kristo Mchungaji mwema anayewapatia: utambulisho, tasaufi na utume wanaopaswa kuutekeleza ndani ya Kanisa.

Kuna matatizo na changamoto nyingi zinazowakumba Wakleri na kwamba, Kanisa halina budi kusoma alama za nyakati, kwa kuibua mbinu na mikakati mipya itakayoliwezesha Kanisa kuendelea kuwa ulimwenguni pamoja na kutekeleza dhamana yake ya Uinjilishaji, katika misingi ya ukweli na uwazi. Kanisa linatambua kwamba, katika miaka ya hivi karibuni limetikiswa kwa kashfa mbali mbali, lakini bado limeendelea kusherehekea vipindi vya umoja na furaha, kwa kuonesha uzuri wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu huu wa utandawazi, kuna hatari kubwa ya baadhi ya watu kujikuta wakiwa wamejifungia katika dhana ya mawazo mepesi mepesi, kwa kuonesha ukavu katika maisha ya kiroho kama ambavyo aliwahi kudokeza Papa mstaafu Benedikto XVI katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2005. Mama Kanisa hana budi kuhakikisha kwamba, anatumia rasilimali na uwezo wake wote katika mchakato wa maboresho ya wito na utambulisho wa maisha na utume wa Kipadre, kwa kufuata nyazo za Kristo mchungaji mwema kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Familia ya Mungu inawahitaji viongozi walipakwa mafuta na Roho Mtakatifu si kwa ajili yao binafsi, bali kwa ajili ya huduma ya upendo, tayari kutoka kimasomaso ili kutangaza na kushuhudia Injili hususan miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni utume unaofumbatwa katika huduma makini kwa kujishikamanisha na Kristo Yesu kwa njia ya sala, tafakari na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Majiundo ya maisha na utume wa Kipadre ni mchakato endelevu unaowajengea Mapadre uwezo wa kuwa kweli ni wafuasi amini wa Kristo Yesu. Ni malezi na majiundo ya: kiakili, kiutu na kiroho. Ikumbukwe kwamba, malezi awali na endelevu yanapaswa kutofautishwa kwani yanagusa maisha ya Kipadre kwa nyakati tofauti, ingawa lengo ni kumuunda Padre mkamilifu. Mapadre wakumbuke kwamba, wameteuliwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya mambo matakatifu; kumbe, wanapaswa kutambua wito na utambulisho wao, tayari kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Wito ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayoimarishwa kwa njia ya malezi ya Jandokasisi tangu mwanzo hadi mwisho wa maisha yake kama Padre, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa ili: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, yote haya ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo! Kardinali Parolin anakaza kusema, haya ni mambo ambayo mabingwa pamoja na viongozi mbali mbali wa Kanisa wamejaribu kuyafanyia kazi wakati wa maadhimisho ya Kongamano kuhusu Nyaraka za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Seminari, Wito na Utambulisho wa Kipadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.