2015-11-23 11:24:00

Kanisa linapaswa kua aminifu kwa Kristo mchumba wake!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 23 Novemba 2015 amelitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linawekeza kwa Kristo Yesu ambaye ni amana na hazina ya milele badala ya kutaliwa na kumezwa na malimwengu kama njia ya kujipata uhakika wa usalama. Mahubiri ya Baba Mtakatifu yamejikita katika Injili ya siku, pale yule mwanamke mjane alipotoa senti yake ya mwisho, hata katika umaskini wake, akaonesha ukarimu kwa Mwenyezi Mungu asili ya mema yote.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwanamke mjane kadiri ya Maandiko Matakatifu ni mtu anayeishi katika hali ngumu na kwamba, anahitaji daima msaada wa jamii inayomzunguka. Mwanamke mjane anayezungumziwa katika Injili ya leo aliwekeza matumaini yake kwa Mwenyezi Mungu; Kanisa linapaswa kuwa na ujasiri wa wanawake wajane, linapongojea ujio wa Kristo ambaye ni hazina yake ya pekee. Hii ni changamoto kwa Kanisa, ambalo kimsingi ni mchumba wa Kristo kuwa aminifu na upendo mkuu kwa Kristo, kinyume chake ni kupoteza dira na mwelekeo na matokeo yake ni kumezwa na malimwengu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata leo hii Yesu Kristo anaendelea kulilia Kanisa lake, ili liweze kuwa ni chemchemi ya maisha mapya kama ilivyokuwa kwa yule mtoto wa mwanamke mjane mjini Naini. Yesu anaendelea kulilia Kanisa lake, ili liweze kupata haki na amani kama alivyoonesha kwenye mfano wa Hakimu dhalimu aliyekuwa anapindisha haki ya mwanamke mjane kwa vile tu hakuwa mchamungu! Moyo wa mwamini unapokuwa karibu zaidi na Yesu, unamwezesha kuyakimbia malimwengu, kumbe hata Kanisa halina budi kujikita katika upendo na uaminifu kwa Kristo Yesu.

Ujane wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu ni hali ambayo inaliwezesha Kanisa kuendelea kua aminifu kwa Kristo Yesu atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu na kamwe lisijitumbukize katika malimwengu, huko litakiona cha mtema kuni. Nyakati hizi za mwisho wa Mwaka wa Liturujia ya Kanisa, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kusali na kumwomba Yesu awasaidie kuwa waaminifu na kuachana na mambo ambayo hayawezi kuwasaidia katika maisha yao ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.