2015-11-21 15:20:00

Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo, Mwaka Mtakatifu na Siku ya Vijana Duniani!


Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linaadhimisha Jubilei ya miaka 1050 tangu Msalaba wa Kristo uliposimikwa nchini humo, kielelezo cha ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti na huo ukawa ni mwanzo wa Ukristo nchini Poland baada ya Mfalme Mieszko wa kwanza kuridhia ujio wa wamissionari kunako mwaka 966. Tangu wakati huo, Poland ikajikuta ikikita mizizi yake katika utamaduni wa Kilatini na kuwa ni sehemu ya Wakristo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linakaza kusema, kwa mara ya kwanza Kanisa nchini humo liliadhimisha Jubilei ya Karne moja tangu Ukristo ulipoingia nchini humo kunako mwaka 1966. Baraka na neema hizi ziliboreshwa zaidi baada ya Yohane Paulo II kuchaguliwa kuliongoza Kanisa na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato mkubwa wa mageuzi nchini Poland, kiasi cha kujipatia tena ushindi na umoja wa kitaifa kunako mwaka 1989.

Maaskofu wanasema kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland yanakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanamwilisha tunu msingi za maisha ya kimaadili, kiroho na kiutu katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Poland katika safari ya maisha yake, imefanikiwa pia kuwa ni wanachama wa Jumuiya ya Ulaya, matunda ambayo Maaskofu Katoliki wa Poland wanapenda kumshukuru Mungu na kumwimbia utenzi wa sifa na utukufu!

Maadhimisho ya kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland yanazinduliwa wakati wa Sherehe ya Kristo Mfalme wa dunia. Huyu ndiye Mfalme ambaye Ufalme wake ni wa milele na wa ulimwengu wote; Ufalme unaosimikwa katika: kweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, amani na mapendo. Jubilei hii itahitimishwa wakati wa Sherehe ya Kristo Mfalme, tarehe 19 Novemba 2016 katika Madhabahu ya Lagiewniki, Jimbo kuu la Cracovia. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Poland kwamba, maadhimisho haya yatasaidia kwa namna ya pekee kabisa kuimarisha mahusiano kati ya waamini na Bikira Maria kwa kukuza Ibada kwa Mama wa Mungu na Kanisa. Hiki ni kipindi cha furaha na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya watakaobahatika kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko wakati atakapotembelea Poland kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.